MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wajasiriamali wa aina mbalimbali nchini katika kujenga na kuboresha zaidi sekta binafsi itakayoshirikiana nayo katika kutoa mchango wenye manufaa makubwa kwa Taifa.
Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 imeielekeza Serikali ihakikisha katika kipindi cha miaka mitano ijayo, watendaji wake wanaendelea kuwa na mtazamo chanya juu ya sekta binafsi na kuishirikisha kikamilifu katika uwekezaji, hususani ujenzi wa viwanda kwa kuimarisha Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini (Blue Print).
Aliyasema hayo jana jioni (Jumapili, Septemba 6, 2020) alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Majengo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akimuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo na wagombea udiwani.
Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kuandaa jukwaa maalumu kwa ajili ya kutangaza vivutio vya uwekezaji vilivyoko ndani ya mkoa huo ili kushawishi wawekezaji kwenda kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda.
Alisema uwepo wa viwanda vingi utasababisha wananchi hususani vijana kupata ajira kwa sababu viwanda vinaajiri watu wengi wenye kada za aina mbalimbali. Pia amewataka vijana kujishughulisha na shughuli mbalimbali zitakazowapatia kipato cha halali na si kusubiri ajira za kutoka Serikalini pekee.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kusimamia nidhamu kwa watumishi wa umma na kudhibiti vitendo vya rushwa ili wananchi wanufaike na kuifurahia nchi yao.
Alisema jukumu kubwa la watumishi wa umma ni kuwatumikia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote, hivyo aliwataka waendelee kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu. Aliwaomba wakazi wa Moshi na Watanzania wawachague wagombea wa CCM ili maendeleo yaendelee kupatikana katika maeneo yao.
“Nimekuja hapa kumuombea kura Rais Dkt. Magufuli. Hakikisheni ifikapo Oktoba 28, 2020 mnapofika katika vituo vya kupigia kura unachukua karatasi ya kupigia kura na kumchagua Rais Dkt. Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano mingine. Mnafahamu vizuri kazi kubwa aliyoifanya miaka mitano iliyopita.”
Waziri Mkuu alisema kuwa, katika kipindi cha miaka mitano ya serikali ya Rais Dkt. Jonh Pombe Magufuli imeweza kuhakikisha inaboresha huduma za afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mkoa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora na kwa ukaribu.
Alizitaja baadhi ya huduma hizo ni pamoja na kuboresha usafiri wa treni na kupunguza gharama kwa wananchi ambapo kwa sasa treni ya abiria kutoka jijini Dar es Salaam hadi Moshi/ Arusha ipo mara nne kwa wiki kwa nauli ya sh. 6,000 tu tofauti na nauli ya basi ambayo ni sh. takribani 40,000. Aidha, usafirishji wa mizigo kwa mwezi umefikia wastani wa tani 1,500 hadi 2,500.
Pia, Waziri Mkuu alitumia mkutano huo kuwakutanisha mgombea ubunge wa CCM jimbo la Moshi Mjini, Tarimo na mtia nia aliyeomba uteuzi wa CCM katika jimbo hilo lakini hakuteuliwa, Ibrahim Shayo ambaye alitamka hadharani kuwa atamuunga mkono mwenzake Tarimo ili kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika jimbo hilo.