Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Polisi Tarakea wilayani Rombo, Septemba 7, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Mgombea wa nafasi ya urais kupitia CCM, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewaomba wakazi wa Tarakea wamchague Profesa. Adolf Mkenda kwa kuwa anauwezo wa kuwatumikia na kuwaletea maendeleo.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Septemba 7, 2020) alipozungumza na wakazi wa Tarakea kupitia simu aliyompigia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Polisi Tarakea, wilaya Rombo, Mkoani Kilimanjaro.
“Watu wa Tarakea nawaomba mumchague Profesa Mkenda msifanye makosa tena. Profesa Mkenda alikuwa Katibu Mkuu wangu na amefanyakazi nzuri na mimi nilimruhusu kwenda kugombea ubunge katika jimbo la Rombo. Rombo nawaomba mnipigie kura, tunataka tulete mabadiliko makubwa nchini.”
Kwa upande wao, wakazi wa Rombo amesema wamefurahishwa sana na heshima kubwa waliyopewa na Rais Dkt. Magufuli hivyo watahakikisha siku ya kupiga kura itakapofika watamchagua yeye pamoja na mgombea ubunge Profesa Mkenda na wagombea udiwani wote kwa tiketi ya CCM.
Mmoja wa wakazi hao Charles Singano amesema anashukuru sana na kumpongeza Rais Dkt. Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kwa Taifa la Tanzania na wananchi wake, ameahidi kumpigia kura na kwamba atahakikisha anawashawishi wakazi wenzake wajitokeze kwa wingi na kumpigia kura.
Naye, Mary Mlai amewaomba akina mama wenzake wamchague Rais Dkt. Magufuli ili waendelee kupata maendelea mazuri zaidi kwa sababu katika kipindi cha miaka mitano ya awali ameweza kufanya mambo mengi ikiwemo kutoa elimu bure, kutetea wanyonge wakiwemo wajane na walemavu.
Awali, Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa huduma bora za afya katika wilaya ya Rombo Serikali ilishatenga sh. bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya kisasa ya wilaya ambapo pia imetenga sh. milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa katika hospitali hiyo.
Kuhusu tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama, Waziri Mkuu alisema Serikali imejenga mradi wa maji Njoro II (Tarakea). “Serikali imekamilisha mradi huu kwa shilingi milioni 200 na unatoa huduma ya maji katika eneo la Tarakea. Malengo ya Serikali kwa sasa ni kutafuta fedha ili kuupanua mradi huo na kuweza kutoa maji katika maeneo mengine ya Tarafa nzima ya Tarekea”
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wa wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro na Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao wamchague Rais Dkt John Pombe Magufuli ili aendeleze kazi ya kuwaletea maendeleo katika maeneo yao ambayo tayari ameshaianza.