……………………………………………………..
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ina fedha za kutosha kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania katika kuboresha huduma za jamii zikiwemo za afya, maji, elimu.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Septemba 7, 2020) alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa soko la Holili wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wakati akimuombea kura Rais Dkt. Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Rombo Profesa Adolf Mkenda na wagombea udiwani kupitia CCM.
Mheshimiwa Majaliwa amewataka wananchi wasifanye mzaha siku ya kupiga kura itakapofika, wasimchague mtu kwa sababu ya ushabiki na badala yake wamchague Rais Dkt. Magufuli na wagombea wote wa CCM ili waweze kushirikiana nao katika kuendeleza miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.
“Tunaomba kura zenu wanaHolili na Watanzania wote kwa Rais Dkt. Magufuli ili akaendelee kuboreshe maendeleo katika sekta ya elimu itakayotuwezesha kuwa na wataalamu wengi. Nawaomba mumchague Dkt. Magufuli kwa sababu ameitendea haki nchi yetu na ni kiongozi mcha Mungu na mpenda maendeleo.”
Akizungumzia kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama inayowakabili wakazi wa Holili, Mheshimiwa Majaliwa amesema tayari Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina kuona namna watakavyoyatoa maji kutoka Ziwa Chala na kuyasambaza kwa wananchi.
Amesema mradi mwingine wa maji unaotekelezwa katika wilaya hiyo ni mradi wa maji Njoro II (Tarakea). “Serikali imekamilisha mradi huu kwa shilingi milioni 200 na unatoa huduma ya maji katika eneo la Tarakea. Malengo ya Serikali kwa sasa ni kutafuta fedha ili kuupanua mradi huo na kuweza kutoa maji katika maeneo mengine ya Tarafa nzima ya Tarekea”
Mheshimiwa Majaliwa amesema mradi wa kijiji cha Ngareni wenye thamani ya shilingi milioni 812.4 uliohusisha ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji la lita 75,000 na ujenzi wa vituo 15 vya kuchota maji pamoja na ufungaji wa bomba za njia kuu na njia za kusambaza maji umekamilika.
Amesema kuwa katika kuhakikisha huduma ya maji na salama inawafikia wakazi wote wa wilaya ya Rombo kikamilifu, Serikali mwezi Julai mwaka huu imevunja Kampuni ya Maji ya Kill Water na kuanzisha Mamlaka ya Maji (ROWASA)