**************************************
Na Karimu Meshack, Sumbawanga
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule alipotembelewa na Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari ofisini kwake leo.
Dkt. Haule ametaja mafanikio yaliyofanywa na Rais wa Awamu ya Tano Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli katika Sekta za Afya, Elimu, Barabara, Umeme, Maji na upatikanaji haki kwa wakati kuwa ni kichocheo cha ujenzi wa amani na utulivu hapa nchini.
“Huduma za jamii kama maji, elimu, umeme, afya, usafiri na usafirishaji ni haki ya msingi ya kila mwananchi. Naipongeza Serikali yangu chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuyapa kipaumbele masuala haya muhimu katika ujenzi wa amani na uchumi wa Taifa kwa kwa ujumla” amesema Dkt Haule.
Mwananchi akipata haki ya maendeleo kwa kuboreshewa na kusogezewa karibu huduma za jamii na nyingine hawezi kujihusisha na migogoro yoyote katika jamii kwani akili yake inakuwa imetulia, hivyo kujielekeza katika kufanya shughuli za maendeleo na kujipatia kipato, ameongeza Dkt. Haule.
Hata hivyo, Dkt. Haule ameiomba Serikali kuendelea kuweka mkazo na juhudi katika kuhakikisha huduma za jamii zinawafikia wananchi wote katika maeneo yao kama inavyojieleza katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025.
Kwa upende wake Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari Bwn. Miraji Magai Maira wakati akimshukuru Mkuu huyo wa Wilaya ya Sumbawanga amesema wanalazimika kufika kwa wananchi na kukutana na makundi mbalimbali ya vinaja, wafugaji, wakulima, Walemavu, viongozi wa Mira na viongozi wa dini kwasababu huko ndiko migogoro inakoanzia na isiposhughulikiwa kwa wakati huhatarisha amani ya nchi.
Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliyoanzishwa Februari, 2012 chini ya itifaki ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari na kuridhiwa na serikali ya Tanzania kupitia Mkataba wa nchi za Maziwa Makuu wa Usalama, Utulivu na Maendeleo itaendelea na mkakati wa utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya kujenga na kudumisha amani na utengamano kwa kufanya vikao vya ujenzi wa amani kwa siku mbili katika mkoa wa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga na baadae kumalizia vikao hivyo mkoani Morogoro.