Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Mhe Dkt John Magufuli inatambua mchango wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini kwa kuisaidia kutoa huduma muhimu kwa jamii kama vile elimu na afya.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa kufunga sherehe za makambi kwa dhehebu la kanisa la waadventista Sabato zilizofanyika katika viwanja vya kanisa hilo mtaa wa Nyakato jijini Mwanza ambapo amelishukuru kanisa kwa kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kutoa huduma kwa jamii kupitia taasisi zake kama vile elimu kwa shule inazozimiliki na huduma za afya zinazotolewa na hospitali zake pamoja na vituo vya afya huku akilipongeza kwa kuungana pamoja na madhebu mengine ya dini katika kuliombea taifa wakati wa janga la ugonjwa wa Covid-19 lililoweka hivi karibuni
”Serikali inatambua, inathamini na inashukuru kwa mchango wenu katika kuleta maendeleo ya nchi ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula akawataka waumini wa kanisa hilo kutumia kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuliombea taifa kuwa na amani na utulivu sanjari na kuchagua viongozi wazuri na wenye hofu ya Mungu kama Rais Mhe Dkt John Magufuli ili nchi iweze kupata maendeleo.
Kwa upande wake Mnenaji Mkuu wa kambi hilo Mchungaji Sadikiel Shehemba akafafanua kuwa kambi la Sabato kwa mwaka wa 2020 lilianza Agosti 30, mwaka huu kabla kuhitimishwa kwake huku likipambwa na kauli mbiu ya _’Mungu Kwanza Mengine Baadae, Yesu anakuja tujiandae’_ sambamba na kusisitiza juu ya ubatizo na umuhimu wake kwa waumini wa kanisa hilo.
Akihitimisha mmoja wa waumini aliyehudhuria kambi hilo Bi Marygoreth John mbali na kuishukuru Serikali kwa kutofungia wananchi wake katika kipindi cha janga la ugonjwa wa Covid-19 kama zilivyofanya baadhi ya nchi akampongeza Naibu Waziri Dkt Mabula kwa namna anavyoshirikiana na jamii yake bila kujali tofauti za kidini, kabila na rangi.