Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kongamano Maalum lililoandaliwa na Kituo cha Radio cha Safina la kuliombea Taifa kwenye uwanja wa Magereza, Kisongo jijini Arusha
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi wa Kituo cha Radio cha Safina cha jijini Arusha , Daniel Lema na mkewe Helen Lema (kulia) wakati alipowasili kwenye uwanja wa Magereza uliopo Kisongo jijini Arusha kushiriki katika Maombi ya kuliombea Taifa yaliyoandaliwa na Kituo cha Radio cha Safina, Septemba 6, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema siri ya Taifa la Tanzania kuendelea kuwa na amani na kimbilio la watu wanaotoka katika nchi ambazo zimepoteza amani ni kwa sababu ya uwepo wa dini, hivyo amewapongeza viongozi wa dini zote nchini kwa kuendelea kuliombea Taifa.
Amesema kuwa kuanzia Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli inaamini kwamba dini ni mkombozi na msingi mkubwa wa amani, mshikamano na utulivu uliopo nchini.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Septemba 6, 2020) katika kongamano maalumu lililoandalia na kituo cha Radio Safina kwa ajili ya kuliombea Taifa na viongozi wake wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu. Kongamano hilo limefanyika katika uwanja wa Magereza Kosongo, Arusha.
“Serikali itaendelea kushirikiana na dini zote na Rais Dkt. Magufuli anaamini kwamba dini inamchango mkubwa katika kulifanya Taifa kuendelea kuwa ana amani. Nawashukuru viongozi wa dini nchini kwa kuliombea Taifa na kulifanya liepukane na vikwazo vingi ambavyo vingeleta athari.”
Waziri Mkuu amesema nchi iliokolewa kutoka katika majanga mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa corona ambao bado umeendelea kuyasumbua mataifa makubwa yenye uwezo na nguvu duniani kutokana na maombi yaliyofanywa na dini zote baada ya Rais Dkt. Magufuli kuwaomba Watanzania wafunge siku tatu kumuomba Mwenyezi Mungu aliepushe Taifa na ugonjwa huo.
Ametumia fursa hiyo kuwasihi viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla waendelee kushirikiana katika kuliombea Taifa na wamuombe Mwenyezi Mungu aiepushe Tanzania na majanga ili nchi iendelee kuwa na amani.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, 2020, Waziri Mkuu amesema siku ikifika wajitokeze kwa wingi na wakachague viongozi bora watakaoweza kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Kimanta amewahakikishia wananchi wa mkoa huo kwamba mkoa upo salama na kwamba wajitokeze kwa wiki kushiriki katika kampeni na wasikubali kutishwa na mtu yeyote.
Mkuu huyo wa mkoa aliongeza kwa kuwasihi wananchi wa Arusha kamwe wasikubali kudanganywa na watu wasioutakia mema mkoa wao na Taifa kwa ujumla. “Tunzeni kadi zenu za kupigia kuwa ili wakati utakapofika muweze kuchagua viongozi bora.”
Awali, Mama Hellen Lema ambaye ni Mkurugenzi wa Radio Safina iliyoandaa kongamano hilo amesema licha ya kuliombea Taifa na viongozi wake pia, kongamano hilo lililotanguliwa na maombi yaliyofanyika kwa siku 21 linalenga kuvunja madhabahu yaliyokuwa yawakandamiza watu kwa muda mrefu.