Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole akiongea na wafugaji katika moja kati ya kambi iliyopo pori la Mkowela wilayani humo akiwa katika kampeni ya uelimishaji na uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa jamii ya wafugaji hao.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole akiwa na baadhi ya wataalam na viongozi wa kijiji cha Majala walipokwenda katika kambi mojawapo ya wafugaji umbali wa km 20 kwa ajili ya kutoa elimu na uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu hasa baada ya kubainika kwamba jamii ya wafugaji ni kati ya makundi yaliyopo katika hatari ya kupata TB kutokana na kunywa maziwa yasiochemshwa vizuri.
Picha na Mpiga Picha Wetu,
………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Tunduru
KUTOKANA na wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma kuwa na muingiliano mkubwa wa wafugaji kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini,kitengo cha kifua kikuu na ukoma wilayani humo kimeanza kuwatembelea wafugaji hao katika maeneo wanayoishi kuwapima ugonjwa wa kifua kikuu na kuwaanzishia dawa wale watakaobainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema, wameanza kuwafuata wafugaji baada ya kubainika kwamba jamii ya wafugaji Iko katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu kutokana na baadhi yao kunywa maziwa yasiochemshwa vizuri na ng’ombe alikuwa na wadudu wa Tb.
Mkasange alisema kutokana na hatari hiyo kwa wafugaji, ndiyo maana Hospitali ya wilaya ya Tunduru kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kimeanza mkakati wa kuwatembelea wafugaji wote ambao wanaishi mbalimbali na maeneo ya kutolea huduma kwa lengo la kuwapa elimu,kufanya uchunguzi na kuwaanzishia dawa.
Kwa mujibu wa Kihongole,mkakati huo utasaidia sana jamii ya wafugaji kufahamu ugonjwa wa kifua kikuu na namna ya kuchukua tahadhari hasa ikizingatia kuwa, wafugaji wengi wanaishi na kufanya shughuli zao mahali ambako sio jambo rahisi kufikiwa na huduma za kijamii ikiwemo vituo vya kutolea huduma.
Alisema, mkakati wa kitengo cha kifua kikuu kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma ya uchunguzi bila kujali mahali anapoishi na ni haki ya kila mmoja kupata matibabu kama mpango wa Serikali ya awamu ya tano.
Mkasange ambaye ni mratibu wa tiba asili na tiba mbadala wa wilaya ya Tunduru,amewataka wafugaji kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kupima mifugo yao mara kwa mara na wanakunywa maziwa yaliyochemshwa vizuri badala ya kuendelea na utamaduni wa kunywa maziwa mabichi ili kuepuka uwezekano wa kupata maambukizi ya kifua kikuu.
Aidha amewashauri wafugaji hao kuanza kujenga nyumba bora zitakazo ruhusu kupitisha mwanga hewa nyingi na mwanga mkubwa badala ya kuishi kwenye maboma ambayo hayana hewa na mwanga wa kutosha kwa sababu wadudu wa kifua kikuu upenda kuishi gizani na maeneo yenye hewa hafifu.
Aidha Mkaange ameionya jamii kuepuka kutumia dawa ovyo bila kufuata ushauri wa wataalam kwani tabia hiyo imekuwa chanzo cha kukithiri kwa magonjwa sugu yanayosababishwa na matumizi holela ya dawa.
Katika kampeni hiyo wataalam kutoka kitengo cha kifua kikuu wametembea kambi mbili za wafugaji eneo la Mkowela na Majala umbali wa zaidi ya km 50 kuwafuata wafugaji.
Wakizungumzia huduma hiyo,baadhi ya wafugaji wameipongeza Hospitali ya wilaya Tunduru kupitia kitengo cha kifua kikuu kwa hatua hiyo ambapo walisema, itawezesha kufahamu ugonjwa wa kifua kikuu na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ambao unatajwa kati ya magonjwa kumi yanayoongoza kupoteza maisha ya watu wengi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Majala Hussein Kilalo ameishukuru Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu kwa kitendo cha kuwafuata wafugaji hao kwa ajili ya kupeleka elimu na kuwapima wafugaji ugonjwa wa kifua kikuu.
Hata hivyo,ameiomba Serikali kukiongezea nguvu kwa kupeleka huduma za Afya jirani na wafugaji na wananchi wanaoishi mbali na maeneo ya kutolea huduma ambao wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata matibabu.