Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akizungumza na Watumishi na wananchi wilayani Ngorongoro kabla ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro Septemba 04, 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akizindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro Septemba 04, 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akikata utepe kufungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro Septemba 04, 2020. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Rashid Taka na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Bibi Sabina Seja.
Baadhi ya Watumishi na wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika alipokuwa akizungumza nao kabla ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilayani humo Septemba 04, 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akizungumza na Viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro ofisini kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Rashid Taka (wa kwanza kulia kwa Mhe. Waziri) alipoitembelea Ofisi hiyo kabla ya kufungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro Septemba 04, 2020.
Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Bibi Sabina Seja akitoa maelezo ya awali kuhusu jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ngorongoro kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika kuzungumza na wananchi na kulizindua jengo hilo Septemba 04, 2020.
**************************************
Na. Mary Mwakapenda-Ngorongoro
Tarehe 04 Septemba, 2020
Watanzania wameaswa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa kwa kuzitumia vizuri Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini ili kuwa chachu ya maendeleo kwenye jamii wanayoishi, ikizingatiwa kuwa rushwa ikishamiri katika taifa lolote lile huwa ni kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika wakati akiwasihi wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro kuitumia vizuri Ofisi ya TAKUKURU wilayani humo, aliyoizindua rasmi Septemba 4, 2020.
Mhe. Mkuchika amesema, njia sahihi ya kuleta maendeleo nchini ni ushiriki wa kila Mtanzania kuwafichua wala rushwa na kutoshiriki vitendo vya rushwa, hususani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ambao taifa linategemea kupata viongozi bora wenye nia ya dhati ya kuleta maendeleo.
Msishawishike kuomba rushwa wala kupokea rushwa kwa lengo la kumchagua kiongozi wa chama chochote kile cha siasa”, Mhe. Mkuchika amewaasa wananchi na kuongeza kuwa, uchaguzi ukigubikwa na vitendo vya rushwa hautakuwa na tija kwa maendeleo ya taifa.
Aidha, kuhusu azma ya Serikali kuokoa fedha za umma, Mhe. Mkuchika ameipongeza TAKUKURU Mkoa wa Arusha kwa kuokoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 2,490,396,226.00 katika kipindi cha mwaka 2019/2020, fedha ambazo zitatumika kikamilifu kwenye miradi ya maendeleo.
Kama mnavyofahamu mtazamo wa mataifa kwa sasa ni kurejesha Serikalini mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa na ubadhirifu ili zitumike kwenye shughuli za maendeleo.” Mhe. Mkuchika amefafanua.
Mhe. Mkuchika ameahidi kuwa, Serikali itahakikisha TAKUKURU inaendelea kuimarika, hivyo amewataka Watumishi wa TAKUKURU kuongeza juhudi katika kutekeleza jukumu lao la kuzuia na kupambana na rushwa nchini.
Akitoa maelezo ya awali, Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bibi Sabina Seja amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwajengea ofisi na kuwapatia rasilimali za kutosha, hivyo ameahidi kuwa TAKUKURU itafanya kazi kwa bidii kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa nchini.
Ufunguzi wa jengo la Ofisi ya TAKUKURU Ngorongoro ni ushahidi wa namna Serikali ilivyodhamiria kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuiwezesha TAKUKURU kuwa na ofisi itakayorahisisha utendaji kazi wake.