MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imetekeleza miradi ya maji 1,423 yenye thamani ya sh. trilioni 1.2 katika miji 28 nchini ikiwemo na wilaya ya Longido.
Amesema upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama vijijini umeongezeka kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 70 mwaka 2020 na kwa mijini kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2020.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 3, 2020) alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Polisi wilayani Longido mkoani Arusha wakati akimuombea kura Rais Dkt. Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Longido Dkt Stephen Kiluswa.
“Jambo kubwa lililokuwa linasumbua Longido ni upatikanaji wa maji safi na salama, Serikali iliamua kutoa sh. bilioni 15.8 kwa ajili ya mradi wa majisafi mji wa Longido ambao utahudumia mji wa longido na vitongoji vyake. Mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wanapata maji.”
Amesema mbali ya mradi huo mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Simba mkoani Kilimanjaro hadi Longido pia, Serikali imetoa sh. bilioni 4.5 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa majisafi katika mji wa Namanga wilayani Longido na usanifu wa mradi huo umekamilika.
Pia, Waziri Mkuu amesema jumla ya sh. bilioni 12.0 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji vya Tingatinga, Ngereyani, Noondoto, Irkaswa, Kamwanga, Mairowa, Karao, Lesing’ita, Mundara na Orgira wilayani Longido.
Amesema lengo la Serikali ya CCM kutekeleza miradi hiyo ni kutaka kuhakikisha kila kijiji nchini kinakuwa na maji ya kutosha. “Maji lazima yatoshe na ndio sababu ya Rais Dkt. Magufuli kuanzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani na kazi hiyo ameifanya.”
Waziri Mkuu amewaomba wananchi wa wilaya ya Longido na Tanzania kwa ujuma wahakikishe wanampiga kura za kutosha Rais Dkt. John Pombe Magufuli na wagombea wake wote katika ngazi ya ubunge na udiwani nchini.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewapongeza wananchi wa wilaya ya Longido kwa kutambua mchango mkubwa wa maendeleo uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwapitisha wagombea udiwani wa CCM katika kata zote 18 za wilaya hiyo bila ya kupingwa.
Pia, Waziri Mkuu amewataka madiwani hao wahakikishe wanazunguka katika vitongoji vyote vya wilaya hiyo kwa ajili ya kuomba kura za Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mgombea wa nafasi ya ubunge Dkt. Kiluswa.