***********************************
Na Mwandishi wetu, Babati
MMILIKI wa kampuni ya JACO Service Group John Stepheni Kabelinde maarufu kama Babu Joha ambaye ni mkazi wa jiji la Dar es salaam anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuwasilisha nyaraka za upotoshaji na kujipatia zabuni.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza mjini Babati September 3 mwaka huu amesema Kabelinde anadaiwa kutoa nyaraka hizo na kufanikiwa kupata zabuni ya kufyeka majani yaliyo pembeni ya barabara ya Babati hadi Gehandu.
Makungu amesema Babu Joha alifanikiwa kupata zabuni hiyo kupitia nyaraka za upotoshaji baada ya kuwashinda wazabuni wengine tisa walioomba nafasi hiyo.
Amesema uchunguzi unaonyesha kupitia kampuni yake ya JACO Service Group amekuwa akikwepa kodi mbalimbali za serikali hivyo kuangukia kwenye makosa ya kuhujumu uchumi wa Taifa na anatarajia kufikishwa mahakamani September 4.
Ametumia nafasi hiyo kuvishukuru vyombo vya habari amabayo vimesambaza habari hizo hadi kufanikisha ukamatwaji wa Babu Joha ambaye amekamatwa jijini Dar es salaam.
Awali, Julai 9 mwaka huu Makungu aliwaambia waandishi wa habari kuwa Babu Joha anatafutwa na TAKUKURU kwa kudaiwa kufanya kosa hilo hadi hivi sasa ametiwa mbaroni na kusubiri kufikishwa mahakamani.
“Napenda kuwafahamisha watuhumiwa wa uhalifu kuwa serikali ina mikono mirefu hivyo kujificha hakuwezi kuwa suluhisho kwa wanaotafutwa,” amesema Makungu.