Home Mchanganyiko WATUMISHI OFISI YA RAIS-UTUMISHI WAPATIWA MAFUNZO KUONGEZA WELEDI NA UFANISI ILI KUBORESHA...

WATUMISHI OFISI YA RAIS-UTUMISHI WAPATIWA MAFUNZO KUONGEZA WELEDI NA UFANISI ILI KUBORESHA UTOAJI HUDUMA

0

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa ofisi yake (hawapo pichani) yenye lengo la kuwajengea uwezo kiutendaji ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifurahia ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa uandishi wa nyaraka za ofisi, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, mapambano dhidi ya rushwa pamoja na namna bora ya kukabiliana na msongo wa mawazo mahala pa kazi.

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Mwanaheri Cheyo akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa ofisi hiyo yaliyoanza Septemba 2, 2020 katika Ukumbi wa UDOM na yatahitimishwa Septemba 4, 2020.

*************************************

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 02 Septemba, 2020.

Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB) wapatiwa mafunzo yatakayowawezesha kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na ufanisi ili kuboresha utoaji huduma kwa umma na wadau wengine wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Hayo yamesemwa leo na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa ofisi yake yatakayotoa fursa ya kuwajengea uwezo kwenye eneo la uandishi wa nyaraka za ofisi, utunzaji bora wa kumbukumbu na nyaraka, mapambano dhidi ya rushwa ikiwa ni pamoja na namna bora ya kukabiliana na msongo wa mawazo mahala pa kazi.

Dkt. Michael amewaka watumishi hao kufuatilia kwa umakini mafunzo hayo ili wapate elimu na weledi kuhusu namna bora ya uandishi wa nyaraka, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, kuepuka vitendo vya rushwa na msongo wa mawazo ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaweza kuathiri utendaji kazi wao wa kila siku.

“Mafunzo haya ni muhimu katika kuiwezesha ofisi kupata watumishi mahiri, waadilifu, wenye kuzingatia weledi na ufanisi kiutendaji”, Dkt. Michael amesisitiza.

Dkt. Michael amefafanua kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kama zilivyo taasisi nyingine nyeti, inapaswa kuwa na watumishi bora na wenye ujuzi na maarifa yatakayowaongezea ufanisi kiutendaji na ndio maana menejimenti imeamua kuwapatia mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wengine.

Mafunzo haya ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wa OR-MUUUB yanafanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kuanzia tarehe 02 hadi 04/09/2020 na yatahudhuriwa na watumishi 218.