*****************************************
NA MWAMVUA MWINYI, PWANI
MGOMBEA Udiwani Kata ya Miono, Chalinze ,Bagamoyo, Juma Mpwimbwi, amemuomba Katibu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi Abdurhman Kinana amfikishie kilio cha Barabara ya Afrika Mashariki mgombea Urais Dkt. John Magufuli.
Pamoja na barabara hiyo,Mpwimbwi amezungumzia adha katika barabara ya Saadani mpaka Mandera, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitengenezwa kwa kiwango cha changarawe, hali inayosababisha kuharibika kila wakati.
Mpwimbwi anayetetea nafasi hiyo, alitoa rai hiyo kwa Kinana, kwenye uzinduzi wa Kampeni jimboni humo, uliofanyika Miono, ambayo mgeni rasmi alikuwa Kinana, ambapo alipomkabidhi kipaza sauti kwa niaba ya madiwani wenzake, alielezea kilio hicho huku akimuomba akifikishe kwa Magufuli.
“Nina furaha kubwa ya kusimama mbele yako kiongozi wangu mkubwa katika chama na serikali yetu katika awamu zilizopita, kwanza niishukuru Serikali awamu zote kwa kazi kubwa ilizozifanya, lakini kipekee kabisa ya awamu ya tano, kazi kubwa inafanyaka, tunakuomba utufikishie kilio hiki,” alisema Mpwimbwi anayetetea nafasi hiyo.
Nae mgombea ubunge jimboni humo Ridhiwani Kikwete, alimweleza Kinana kwamba barabara ya Saadani Mandera tayari ipo katika mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami, huku akiwahakikishia wakazi waishio katika maeneo hayo wasiwe na hofu.
“Serikali zetu zimekuwa zikifanyakazi kubwa katika nyanja mbalimbali, kipekee nitumie fursa hii kuwajulisha wana-Miono na Mkange kwamba, barabara za Afrika Mashariki na hii ya Saadani Mandera zipo katika mpango wa kutengenezwa kwa kiwango cha lami,” alisema Ridhiwani.
Aliongeza kwa kusema kuwa wakazi wa maeneo hayo muda si mrefu watakuwa kwenye maeneo ya kupendeza kutokana na ujenzi huo wa kiwango cha lami, hatua itayokwenda kubadilisha mwonekano wa maeneo hayo sanji na hali ya kiuchumi.
Àkizungumza na wana-Bagamoyo, Kinana alisema kwamba suala hilo tayari linafanyiwakazi, huku akiwaomba ifikapo Oktoba wawachague wagombea wanaotokea CCM ili kwa umoja wao waweze kumalizia miradi iliyoanzishwa.