Afisa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya UmojaSwitch Ndugu Danford Mbilinyi ( Kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Halopesa, Ndugu Magesa Wandwi, kwa pamoja wakisaini Mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Halopesa na UmojaSwitch. Akishuhudia Kulia ni Afisa mawasiliano Halotel Bi. Hindu Kanyamala na Kushoto ni Bi. Adellah Kaihula Afisa Masoko wa UmojaSwitch.
Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Halopesa, Ndugu Magesa Wandwi (kulia) akiongea na waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa huduma ya kutoa pesa kwenye ATM za Umoja katika makao makuu ya Ofisi za Halotel Dar es salaam,alisema Huduma hiyo itawawezesha wateja wote wa Halopesa kutoa pesa kupitia ATM zote za Umoja. Kushoto ni Afisa Mkurugenzi Mkuu wa UmojaSwitch Ndugu. Danford Mbilinyi.
Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Halopesa, Ndugu Magesa Wandwi (kulia) na Afisa Mkurugenzi Mkuu wa UmojaSwitch Ndugu. Danford Mbilinyi ,wakikabidhiana mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Halopesa na UmojaSwitch, ambapo wateja wa Halopesa nchini wataweza sasa kutoa Pesa katika ATM za umoja zilizopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.Afisa bidhaa na masoko wa Halopesa, Bi.Roxana Kardio akitoa maelekezo jinsi ya kutoa pesa kwenye ATM za Umoja katika mojawapo ya ATM za umoja jijini Dar es Salaam.
*************************************
Taarifa kwa vyombo vya Habari.
Dar es Salaam, 02 Septemba, 2020, Kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia na uchumi, Halopesa imeendelea kutanua wigo wa kutoa huduma zake za kifedha nchini ikizingatia pia mkakati wa kitaifa wa ujumuishwaji wa wananchi katika matumizi ya mifumo rasmi ya kifedha chini.
Ikiwa ni mwendelezo wa kuwafikia na kuwapa wateja wa Halopesa huduma bora kwa urahisi na uhakika, Halotel kupitia Huduma yake ya HaloPesa imeingia ubia na Kampuni ya UmojaSwitch kutoa huduma kwa wateja wa HaloPesa ya kutoa fedha kupitia ATM za Umoja zilizoko kote nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hii katika ofisi za Makao Makuu ya Halotel, Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Halopesa Ndugu , Magesa Wandwi, amesema kuwa ni hamasa na lengo letu kuhakikisha kuwa tunaendelea kutumia miundo mbinu ya teknolojia na fursa zote zilizopo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta hii ya huduma za kifedha na kuwapa wateja wetu huduma bora na za uhakika na nifuraha yetu leo kushirikiana na UmojaSwitch kuzindua rasmi huduma hii ambayo itawawezesha wateja wa HaloPesa kutoa fedha kwa urahisi na uhakika zaidi kupitia ATM za Umoja zaidi ya 250 zilizopo maeneo mbalimbali kote nchini.
Tunapenda kuwasisitizia wateja wetu kuwa Huduma hii haitakuwa na makato ya ziada tofauti na makato ya kawaida ya kutoa pesa kwa wakala wa kawaida, lakini pia huduma hii haitahusisha matumizi ya internet pale ambapo mteja atakuwa anatoa fedha kwenye ATM za Umoja, aliongeza Magesa.
Kwa Huduma hii pamoja na mawakala wetu zaidi ya Elfu Hamsini (50,000) waliosambaa nchini kote kwa pamoja tutaendelea kuwahudumia wateja wetu wa Halopesa zaidi ya Milioni Mbili (2,000,000) waliopo mijini na vijijini.
Mteja wa Halopesa atapitia hatua za kawaida kutoa pesa kwa kupiga *150*88# kisha kuchagua ‘2’, (Kutoa Pesa ), Kisha chagua tena “2” (UmojaATM), ataendelea na kuweka kiasi na namba yake ya siri ya Halopesa, baada ya hapo atapata ujumbe wenye namba ya siri ya uthibitisho ambayo ataitumia kutoa fedha katika ATM za Umoja. Aliongeza Magesa.
Akiongea na waandishi wa Habari katika uzinduzi huo, Mkurugenzi mkuu wa UmojaSwitch, Ndugu. Danford Mbilinyi, alisema ushirikiano na Halopesa utaongeza upatikani wa huduma za kifedha kirahisi nchini kupitia ATM zetu zaidi ya 250 zilizoenea nchi nzima na kwamba wateja wa HaloPesa wana fursa nyingine ya uhakika sasa ya kupata fedha muda wowote mahali popote nchini.