Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) Ireen Mark wa katikati , Amemtaka Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe kuomba radhi waandishi wa TBC waliyofukuzwa wakati wa ufunguzi wa kampeni za chama hicho jijini Dar es salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama hicho Siyovelwa Hussein na kulia ni Mweka hazina Patricia Kimelemeta.
***********************************
Ijumaa ya tarehe 28/08/2020 Ulimwengu wa Wanahabari na Watanzania kwa ujumla ulipigwa na butwaa pale Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Freeman Alkaeli Mbowe, alipoamrisha waandishi wa habari wa televisheni ya Taifa (TBC) kuondoka katika mkutano wa ufunguzi wa kampeni za chama hicho, uliofanyika kwenye viwanja vya Mbagala Zackem jijini Dar es Salama kwa tuhuma za kwamba wanafikiri wao ni televisheni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika amri yake Mhe. Mbowe alitoa dakika 15. Kwa waandishi hao kuwa wamefunga vyombo vyao na kuondoka katika eneo la mkutano huo kwa madai kwamba TBC ilikuwa imesitisha matangazo ya mkutano huo ambayo awali yalikuwa yakirushwa mubashara.
Mbowe alisema wamechoka kuonewa na kufanywa wapumbavu hivyo aliwapa dakika 15 wawe wameondoka kwenye viwanja vya mkutano.
Kwa vipimo vyovyote vya kimaadili kitendo hicho kilikosa uungwana na hakikubeba misingi ya kiutu hata kama zilikuwepo dalili zozote za kukatishwa kwa matangazo hayo au huko kufanywa wapumbavu kama alivyosema Mhe. Mbowe.
Kitendo kile ambacho kilikosa busara na ukomavu wa kisiasa siyo tu kiliwadhalilisha na kuwafedhesha waandishi wale pamoja na taaluma yao isipokuwa zaidi kilihatarisha usalama wao na vifaa vyao kutokana na mazingira yaliyokuwepo.
Kutokana na hali hiyo ambayo haivumiliki hasa katika kipindi hiki cha kampeni za kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020 sisi DCPC ni klabu huru ya waandishi wa habari mkoa wa Dar es salaam, wakati tukiendelea kutafakari hatua sahihi za kuchukua kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari mkoani humu, inachukua nafasi hii kukemea na kulaani kitendo kile pamoja na kumtaka Mhe. Mbowe kuomba radhi kwa waandishi wale, Televisheni ya taifa, tasnia ya habari, pamoja na Watanzania kwa ujumla.
Tasnia ya habari ni nyenzo muhimu katika upashanaji wa habari hasa nyakati hizi za kampeni za kisiasa na uchaguzi wananchi wanahitaji kujua sera, ilani na mipango ya vyama vya siasa kabla ya kupigakura. Na kwa vyovyote hakuna njia rahisi ya wananchi kuyapata yote hayo kama si kupitia vyombo vya habari ambavyo CHADEMA imeamua kuwadhalilisha.
DCPC inaungana na vyombo, taasisi na watu wote ambao wamekerwa na kitendo kile na inaviasa vyama vingine vyote kujiepusha na mihemuko inayoweza siyo tu kudhalilisha taaluma ya habari lakini pia kuwatia hatarini waandishi wa habari wanapokuwa kazini.