……………………………………………….
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Sikusudii kuamsha upya hisia za huzuni zilizotugubika mara tu baada ya kusikia taarifa ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli akitangazia umma juu ya kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa kilichotokea usiku wa kuamkia Julai 24, 2020.
Ni dhahiri kuwa kifo cha Rais huyo mstaafu na mwanadiplomasia mkongwe ni pigo kwa taifa, Afrika pamoja na dunia kufuatia mchango wake ulioakisi mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa, mahusiano ya kimataifa na mapinduzi katika sekta za umma na binafsi nchini.
Hakika, watanzania hawana budi kujifunza mambo mengi aliyoyafanya Mzee Mkapa na pia kumuenzi kwa kuthamini mchango wake uliosaidia kuleta mabadiliko katika kuleta maendeleo ya kijamii, kiasiasa na kiuchumi.
Katika uongozi wake mzee Mkapa alianzisha mikakati ya kimaendeleo kwa jamii katika nyanja mbalimbali. Nyanja mojawapo ambayo chini ya uongozi wake iliandaliwa kimkakati ni uendelezaji wa sanaa na muziki.
Kama tunavyokumbuka, sekta ya sanaa na muziki kwa miaka mingi imekuwa na changamoto nyingi hususan kuwepo kwa dhuluma kwa wasanii na wanamuziki ambao wamekuwa wakitegemea kazi zao kwa lengo la kujipatia kipato. Wamekuwa wakitengeneza filamu na kutunga nyimbo ambazo hazikuwanufaisha wasanii kutoka na kudhulumiwa , sababu kubwa ikiwa ni kukosekana kwa Sheria ya Hakimiliki.
Kutokana na kilio cha muda mrefu cha wasanii na wanamuziki kwa kuibiwa kwa kazi zao, mzee Mkapa alianzisha Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), chombo ambacho ni cha kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 46 cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Namba 7 ya mwaka 1999.
Chombo hiki kimepewa mamlaka ya kusimamia Sheria ya Hakimiliki. Hatua hii ilikuwa ni mwanzo wa safari ndefu ya wasanii na wanamuziki katika kuwaletea mafanikio makubwa ikilinganishwa na sheria ya zamani ambayo miongoni mwa mambo mengine, haikuweka kipengele cha kusimamia Hakimiliki za wasanii na wanamuziki.
Licha ya kusimamia Hakimiliki, kazi nyingine za COSOTA ni kukuza na kulinda maslahi ya waandishi wa vitabu, waigizaji, wafasiri, wachapishaji, watengenezaji wa rekodi za santuri, watangazaji na wachapishaji na hasa kukusanya na kusambaza mirabaha yoyote na malipo mengine yanayostahili kuhusiana na haki zao. Aidha, chama hiki pia ni kiungo kati ya wamiliki wa haki kwa upande mmoja na watumiaji wa kazi zao kwa upande mwingine.
Ni dhahiri shahiri kuwa Mzee Mkapa alizingatia maslahi mapana ya watu wanaojihusisha na kazi za sanaa, uandishi na utangazaji na hivyo kutokana na kifo chake watanzania tuna kila sababu ya kuendeleza kila zuri alilolifanya. Sambamba na kujifunza namna bora ya kuendeleza vipaji, kazi za sanaa na kila mmoja kuchangia kwa namna yake kwa lengo la kuboresha maisha katika jamii, kupunguza umasikini kama yalivyokuwa maono yake kwa taifa hili.
Katika kitabu alichoandika Mzee Mkapa miezi kadhaa kabla ya kifo chake na kuzinduliwa na Rais wa Awamu ya Tano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli, alielezea juu ya maisha yake binafsi.
Katika kitabu hicho chenye jina la “Maisha Yangu, Dhamira Yangu: Rais wa Tanzania Akumbuka” Mzee Mkapa alielezea kuwa maono yake ni “maisha ya hali ya juu, amani, utulivu na umoja, utawala bora, jamii iliyoelimika na uchumi shindani wenye uwezo wa kukua kiendelevu na mgawanyo shirikishi wa kipato.”Sasa basi funzo la kifo cha Mzee Mkapa kwa wasanii wa filamu na hasa Bongo movie ni lipi? Ama upi mchango wa Bongo movie kwa taifa?
Mbali na mafunzo yanayopatikana katika filamu za Nsuka, dereva Tax na ile ya Chausiku, ambayo siwezi kusahau kwani ina radha yake ya maisha ya uswazi, au ile ya kitambo ya ushuani ya Girlfriend iliyotoka mwaka 2003 ikiwa ni filamu iliyoleta mapinduzi katika sekta ya uigizaji nchini.
Nadhani wakati umefika sasa watengenezaji wa filamu na wadau wote wa tasnia hiyo wakaanza kuandaa filamu zenye maslahi mapana ya taifa, kuhusu masuala mbalimbali mfano historia ya nchi, maisha ya viongozi mbalimbali kama vile Mama Getrude Mongella namna alivyowakilisha nchi katika Mkutano wa Beijing mwaka 1990, ukombozi wa bara la Afrika na mambo kadha wa kadha.
Hapo bondeni (Afrika ya Kusini) wameandaa filamu kuhusu maisha ya baba wa taifa lao Mzee Nelson Mandela, Marekani wao na filamu zao kama za Barrack Obama, Ton Braxton, Black Panther na ile ya The White house. Nafahamu kuwa wametuzidi kwa teknolojia na taaluma kuhusu uandaaji wa filamu lakini bado naamini hata sisi tuna ubunifu na tunaweza kuandaa filamu zetu kwa teknolojia yetu, mazingira yetu na ubunifu wetu.
Ndugu zangu wa Bongo movie, baada ya kusoma makala hii pengine mtataharuki mkidhani nimewachana kwa ubaya, la hasha! Hakika dhamira yangu ni kuona filamu zetu zinakuwa zaidi ya kuonesha mapenzi na hadithi za kawaida sana. Hakuna ubaya hata kidogo mki-act kuhusu historia ya nchi yetu.
Nchi imepitia matukio mbalimbali,lakini katika filamu zetu kwa kiasi kikubwa maudhui ni yale yale tena utakuta mwanamke wa kijijini eti amevaa wigi, kucha ndefu mithili ya chui, rangi ya mdomo imekolea utadhani ametoka kuchinja kuku kwa mdomo!
Kijana wa kiume mwenye mkorogo, hereni masikioni achilia mbali tattoo zilizomjaa mikononi na miguuni. Kuhusu lugha,hapa nako kunavioja vyake kede kede. Si ajabu wengi wenu mmewahi kuangalia filamu ya Kiswahili lakini jina (tittle) lake limeandikwa kwa lugha ya kingereza. Hebu tujiulize, ni nani amewahi kuangalia filamu ya kihindi yenye jina (title) lililoandikwa kispaniola? Mmeona wapi?
Kuhama kwa COSOTA kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kwenda Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutaakisi mabadiliko yanayohitajika kulingana na wakati uliopo. Ni wazi kuwa watanzania wakiwemo wasanii bado wana majonzi kufuatia kifo cha Mzee Mkapa kutokana na jinsi alivyowaondoa katika unyanyasaji,na dhuluma kwa kuibiwa kwa kazi nyingi walizokuwa wakizifanya kwa jasho lao.
Leo hii watanzania, hususan wasanii wa Bongo movie jiulizeni ni kitu gani cha msingi zaidi ambacho mnakifanya katika kumuenzi Mzee Mkapa? Ni wazi kuwa aliwajali na kuazisha COSOTA ili iwasaidie kulinda kazi zenu sambamba na kuongeza thamani ya vipaji mlivyonavyo ili muweze kupata fedha zitakazowasaidia nyinyi na familia zenu.
Nilisikia na kuona wanamuziki mbalimbali wakiimba nyimbo kuhusu masuala kadha wa kadha aliyoyafanya Mzee wa Uwazi na Ukweli ndani na nje ya urais wake, huenda ilikuwa sehemu muhimu ya kuomboleza wakati wa msiba wake.!
Niwakumbushe tu kuwa na nyinyi mnawajibu wa kuvikumbusha vizazi vya sasa na vijavyo kuwa taifa hili lilipata kuwa na bahati ya kuongozwa na Mzee Benjamin William Mkapa kwani mchango wake katika maendeleo ya taifa hauna kifani. Nasisitiza alikuwa kiongozi adhimu katika taifa hili na hakika ameacha alama itakayoishi milele.
Nafahamu baadhi yenu mtasema kuandaa filamu si sawa na kuandaa muziki, kwa vile filamu inahitaji muda zaidi, ujuzi na raslimali za kutosha ikiwemo fedha. Ni kweli na sahihi kabisa, lakini ni lazima tujiulize kuwa pamoja kutokea matukio mbalimbali katika kipindi cha zaidi ya miaka 50 tangu Uhuru wa nchi hii sekta ya filamu imeweza kuandaa filamu yenye taswira ya nchi ambayo ni urithi kwa vizazi vijavyo na kuitambulisha nchi kimataifa?
Ni wakati sasa mshirikiane na Vyuo Vikuu vinavyotoa taaluma ya sanaa ili kutoa mchango wenu katika taifa. Natambua kuwa wengi wenu ni wasomi tena wenye vipaji. Ni matarajio ya wengi kuona namna mnavyoweza kutumia wasifu na muonekano wenu kwa kuigiza maisha ya mtu kama vile Mzee Mkapa ili kusadifu wasifu wake kwa kutoa mafunzo mbalimbali katika jamii, na hata kufundisha watoto na vijana kuhusu uzalendo.
Kwa namna hiyo najua mtauza filamu zenu na kupata fedha nyingi na muhimu zaidi mtauza historia ya nchi kitaifa na kimataifa na itakuwa such a beakthrough.
Nchi ina matukio mengi yanayoweza kuitangaza Tanzania kimataifa yapo mengi na mazuri ya kujifunza kutoka hapa sio kila kitu kizuri kinatoka ulaya. Kuna historia ya viongozi mashujaa kama vile Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Mtemi Mkwawa, Bibi Titi Mohamed, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, vilevile kuna rasilimali hadhimu mfano Mlima Kilimanjaro, hata kama mmeshindwa kuigiza kwenye filamu zenu kuhusu mlima huu mrefu zaidi barani Afrika basi hata kuutaja kwenye filamu zenu mnashindwa, hapana!
Utadhani ni dhambi, ahhaa… jamani tutasubiri tena hadi Sterve Harvey akosee kuutaja kama Mlima Kilimanjaro uko nchini Tanzania kisha Waziri wa Mali Asili na Utalii apiganie kuueleza ulimwengu kuwa mlima huo uko Tanzania na sio kwa jirani?
Katika hafla ya makabidhiano ya COSOTA yaliyofanyika Julai 15, 2020, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi anasema kuwa taasisi hiyo imejipanga kutekeleza majukumu yake kwa ari mpya na tija katika shughuli za sanaa nchini, sambamba na kuandaa mafunzo maalum ya uandishi wa script ili kuongeza ubora wa filamu.
“Filamu inaonesha mtu anatembea kwa dakika kumi, ili tu filamu ifikishe series mbili au tatu, mnatuchosha watazamani, nataka tuwe na mafunzo ya muendelezo kuhusu uandishi wa script, picha jongefu na picha mnato” anasema Dkt. Abbasi
Niwakumbushe tu kuwa Tanzania ni nchi ya pili ikitanguliwa na Nigeria kwa uzalishaji wa filamu nyingi katika bara la Afrika. Aidha, tuna uwezo wa kutengeneza filamu zenye ubora zaidi kwa kutumia teknolojia iliyopo. ukitazama filamu zinazotengenezwa na mwanamama kutoka nchini Nigeria Mo Abudu kama ile ya The Royal Hibiscus hotel na The Wedding party, utashangazwa na maudhui pamoja na ubora wa filamu hizo, tena kutoka Afrika. iweje watayarishaji wa filamu kutoka Tanzania washindwe?
Nafahamu kuwa filamu bora zinahitaji uwekezaji kuanzia hadithi hadi mandhari za kuvutia, lakini siamini kuwa bila kutengeneza mji maalum kwa ajili ya filamu kama ilivyo Hollywood au Bollywood basi haiwezekani kutengeneza filamu zenye ubora na zitakazovutia soko la kimataifa, si kweli!.
Nchi hii imekuwepo na wanasiasa maridhawa, wanamichezo hodari, wanamuziki mahiri, waandishi wakongwe, utamaduni, raslimali adhimu, mila na desturi kutoka takribani makabila 150 iweje katika miaka zaidi ya 50 ya Uhuru sasa tushindwe hata kuwa na filamu bora zinazoitambulisha Tanzania huko duniani!
Nafahamu itahitaji miaka kadhaa ili kuandaa movies made from the real lives mfano filamu ya Princess Diana, lakini tunaweza kuanza na zile za kabila la wahehe, wahaya, wachaga, wapogolo na wengine, pengine namna shughuli za jando zinavyofanywa ama urithi wa uongozi wa kijadi na nyinginezo.
Hivi karibuni Serikali imeanza utekelezaji wa mipango madhubuti inayolenga kuleta mapinduzi ya sekta ya filamu nchini.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Kiagho Kilonzo anasema kuwa Serikali imeanza kutekeleza mbinu mbalimbali ili kuboresha filamu zinazozalishwa nchini kwa lengo la kufikia soko la kimataifa na kukuza wigo wa ajira nchini.
“Bodi imeanza kukutana na waandaaji wa filamu katika vikao maalumu ambapo tunapitia filamu kwa pamoja na kutoa maoni yanayolenga kuboresha filamu husika na baadae filamu zenye ubora zaidi zinawasilishwa kwenye kumbi za sinema, lengo ni kuongeza ushindani na kuzalisha filamu bora zaidi” anasema Dkt. Kilonzo
Dkt. Kilonzo anataja mkakati mwingine kuwa kuunda kamati maalum itakayosaidia kufuatilia vigezo vya filamu zinazoweza kushiriki tuzo za kimataifa za Oscar ili pia filamu za kitanzania zianze kushiriki tuzo hizo.
Sekta ya filamu inatajwa kuzalisha ajira kwa kiasi kikubwa, ambapo filamu moja inaweza kuzalisha ajira kwa watu 150 hadi 200, ambapo kuanzia mwezi Januari hadi Agosti, 2020 tayari sekta hiyo imezalisha filamu 26 ikiwa ni ongezeko kubwa ukilinganisha na filamu saba tu zilizotengenezwa mwaka 2019.
Fauku ya hayo, Bodi ya Filamu imepokea jumla ya filamu 700 kwa ajili ya ukaguzi kabla ya filamu hizo kusambazwa kwa watazamaji Swali linabaki kwa Bongo movies, je mtaendelea kuongoza katika uzalishaji wa filamu nyingi Afrika ama mtaanza kuzalisha filamu zenye ubora wa viwango vya kimataifa zenye kuakisi historia ya nchi yetu, watu wetu, utajiri na raslimali zetu na mila na desturi zetu?
Mwisho.