*******************************
NA EMMANUEL MBATILO
Klabu ya Yanga imefanikiwa kuwaburudisha mashabiki wake katika kusheherekea kilele cha Siku ya Mwananchi ambapo wamecheza mechi ya kirafiki dhidi ya Aigle Noir kutoka nchini Burudi na kufanikishika kuibamiza mabao 2:0.
Tuisila Kisinda alikuwa mwiba kwa timu ya wapinzani alionesha uwezo mkubwa na kuwafanya mashabiki wamshangilie kwa kelele nyingi hivyo baadae alifanikiwa kupachika bao zuri akipokea pasi kutoka kwa Feisal Salum “Fei toto” mnamo dakika 39.
Kipindi cha pili Yanga walionekana kulemewa licha klabu ya Aigle Noir kucheza pungufu kutokana na mchezaji wao kupewa kadi mbili za njano kipindi cha kwanza.
Yanga ilifanikiwa kupata bao la pili tena kupitia kwa mshambuliaji wao mpya Michael Sarpong mnamo dakika 52 akipokea pasi kutoka kwa Nchimbi.
Nje ya burudani ya mechi hiyo kabambe ya kirafiki, pia kulikuwa na burudani tosha kutoka kwa wasanii kibao akiwemo Harmonize ambaye alitumbuiza nyimbo zake kadhaa.
Harmonize aliingia na mbwembwe zake kwa kutua uwanja wa Mkapa kwa staili ya kamba kitu ambacho kiliwafanya maelfu ya mashabiki kumshangalia.
Muimbaji huyo alitua uwanjani hapo akiwa na watu zaidi 100 , dansa, walinzi pamoja na watu wa sarakasi.