Baadhi ya Vigingi (beacons) zilizohifadhiwa ndani katika mtaa wa Engosowashi, Kata ya Moshono mkoani Arusha badala ya kuchimbiwa ardhini kuonesha mipaka ya kiwanja.
Mpima Ardhi kutoka kikosi kazi maalum cha Wizara ya Ardhi bibi Cresencia Thomas akiwa na mpima kutoka Kampuni ya Savei Consult wakikagua uwekaji wa vigingi (beacons) katika mipaka ya viwanja na uchoraji wa ramani za upimaji (survey plan).
Mpima Ardhi kutoka kikosi kazi maalum cha Wizara ya Ardhi bibi Cresencia Thomas akiwa na mpima kutoka Kampuni ya Savei Consult wakikagua uwekaji wa vigingi (beacons) katika mipaka ya viwanja na uchoraji wa ramani za upimaji (survey plan).
Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Engosowashi wakiwa katika mkutano wa uhamasishaji kwa ajili ya urasimishaji unaondelea kwenye mtaa huo uliopo Kata ya Moshono mkoani Arusha.
**************************************
Warasimishaji wanaofanya kazi za upangaji na upimaji makazi holela katika mitaa mbalimbali ya mkoa wa Arusha wameagizwa kufanya kazi hizo kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma zao ili kazi zao zikidhi vigezo vya upangaji na upimaji vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria.
Maagizo hayo yametolewa na Bwn PrayGod Shao, Kiongozi wa kikosi kazi maalum cha Wizara ya Ardhi, kilichoundwa kwa ajili ya kukwamua changamoto za urasimishaji mkoani Arusha wakati alipokuwa akikagua kazi za upimaji katika Mtaa wa Engosowashi Kata ya Moshono na Mtaa wa Olmokea Kata ya Sinoni.
Akiwa katika ukaguzi wa uwekaji vigingi (beacons) na uandaaji wa ramani za upimaji (survey plan), Bwn Shao amesema amegundua warasimishaji wengi hawafuati sheria na kanuni za upimaji kwani badala ya kupanda vigingi kwenye mipaka ya viwanja wamevikusanya na kuvifungia ndani ya nyumba kitu ambacho ni kinyume na sheria ya upimaji.
‘Vigingi (beacons) vinatakiwa vichimbiwe chini ardhini ili vitumike kama alama ya kubainisha mpaka wa kiwanja kimoja na kingine na siyo kuhifadhiwa ndani, alisema Shao.’
Aidha, Bwn Shao aliongeza kwamba, mbali na kuvifungia ndani vigingi walivyopaswa kuvichimbia ardhini, bado wameweka alama hewa za upimaji kwenye ramani (Survey plan) ambapo utakuta ramani inaonesha kiwanja kimewekewa vigingi ila ukifika kwenye kiwanja husika hakuna uhalisia wa vigingi hivyo.
Alisisitiza kwamba, serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya kusimamia ardhi haiwezi kufumbia macho udanganyifu kama huo unaofanywa na warasimishaji wa kuweka alama hewa za upimaji katika viwanja kwa sababu mwisho utasababisha migogoro isiyo ya lazima. Ni lazima sheria na miongozo ya upimaji izingatiwe kwa kuhakikisha kila kiwanja kiwekewe vigingi vyake na ramani inasomeka vivyo hivyo.
Kwa upande wake msimamizi wa Kampuni ya Savei Consult moja kati ya Kampuni zinazofanya urasimishaji katika mkoa wa Arusha Bwn Bryson Michael alisema, uwekaji vigingi (beacons) kwenye mitaa yote ya urasimishaji unasua sua kutokana na mwitikio mdogo wa wananchi wa kulipa gharama za upimaji kiasi cha Tsh. 150,000 kilichowekwa na Serikali.
Bryson alisema, kazi ya utambuzi wa makazi katika mitaa mitatu kwenye Kata ya Moshono aliyopewa kurasimisha imeshafanyika ambapo michoro ya mipangomiji kwa mitaa hiyo imeshaandaliwa na hivyo upimaji unaendelea.
Kwa kuona umuhimu wa kazi ya urasimishaji mkoani Arusha, Wizara ya Ardhi iliunda kikosi kazi maalum cha kufuatilia na kukwamua changamoto za urasimishaji, na kilianza kazi tangu Agosti 17, mwaka 2020 ambapo kufikia Agosti 30, mwaka huu 2020 makampuni yote yaliyokuwa yanafanya urasimishaji katika Mkoa wa Arusha yanapaswa kukamilisha kazi zao zote.