*****************************************
Na Mwandishi Wetu, Mtwara.
Katika kuhakikisha azma ya Serikali ya kuendeleza na kukuza uchumi wa Viwanda, Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC kimesema ipo haja kwa Wawekezaji kukitumia kituo hicho katika kufanikisha shughuli zao ambazo ndio chachu ya ukuaji wa uchumi huo.
Kituo hicho ambacho kinaratibu, kuhamasisha na kusimamia Uwekezaji nchini sasa kinafanya jitihada za kuwatembelea Wawekezaji kwenye maeneo ya uwekezaji wao ili kukagua na kutatua changamoto zinazowakabili.
Mkurugenzi wa Kituo hicho Dkt Maduhu Kazi aliwatembelea Wawekezaji Mkoani Mtwara ambapo akiwa katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote,alisema lengo ni kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kushirikiana na Wawekezaji pamoja na Wadau wa Sekta mbalimbali za Serikali na Binafsi zinazohusika na uwekezaji katika kufanikisha shughuli hizo nchini.
“Nawapongeza sana Wawekezaji wa Kiwanda hiki cha Dangote, mnafanya kazi nzuri katika uwekezaji wenu, sisi TIC tupo kwa ajili yenu, kitumieni kituo hiki kwa maendeleo ya Uwekezaji katika nchi yetu na sisi tupo tayari kuwahudumia wawekezaji wote ili kukidhi matarajio ya nchi katika ukuaji wa uchumi” alisema Dkt Kazi.
Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote Bw. Aboyomi Awofodu amesema kwa sasa kiwanda hicho kinafunga mitambo ya kisasa itakayowezesha kutumia umeme wa gesi, makaa ya mawe na maji ili kuwa na umeme wa uhakika wakati wote.
Kiwanda cha Saruji cha Dangote chenye eneo la ekari 1,700 kilichopo katika eneo la Msijute katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ni moja ya Uwekezaji Mkubwa Nchini Tanzania, Kiwanda hiki ni kikubwa katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara na kina uwezo wa kuzalisha tani za saruji milioni tatu kwa mwaka.
Kiwanda hiki kilianza kazi Desemba 2015 na hadi sasa kiwanda hicho kinazalisha saruji ya kiwango cha daraja la 32.5 na 42.5 ambayo inatumika nchini na nyingine kusafirishwa nje ya nchi, hivi karibuni Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani alizindua mradi wa kwanza wa kuunganisha miundombinu ua gesi asilia katika kiwanda hicho kwa ajili ya kuzalisha umeme wa megawati 45, Mmiliki wa kiwanda hicho ni Raia wa Nigeria Alhaj Aliko Dangote.