***********************************
Na Mwandishi wetu,
Mtwara.
August 27, 2020.
Mkoa wa Mtwara unaendelea kuimarisha miundombinu inayochangia kukua kwa uwekezaji ikiwepo upanuzi wa Bandari ya Mkoa huo uliogharimu shilingi Bilioni 157 na ujenzi wa njia nyingine ya kurukia ndege unaogharimu sh. Bilioni 50.
Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Alphayo Kidata alisema lengo la ujenzi wa miundombinu hiyo ni kuhakikisha Mkoa huo unafungua njia zake za kiuchumi hususan kwenye Kilimo cha zao la Korosho na uwepo wa gesi asilia ambayo imekuwa chachu ya uanzishwaji wa viwanda ambavyo vimekuwa na tija ya kiuchumi.
Kidata aliyasema hayo Mkoani Mtwara wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt. Maduhu Kazi alipotembelea Mkoa huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika Kanda ya Kusini yenye lengo la kuangalia fursa na changamoto za Uwekezaji.
“Mtwara tumejipanga kupokea Uwekezaji, tunao Wawekezaji wanaofanya vizuri na tunazidi kukaribisha wengine wengi, tunazo fursa na miundombinu yote, pia kwa sasa tunaendelea kuimarisha ujenzi wa miundombinu mingine ya kisasa ya usafirishaji ikiwepo Bandari na Uwanja wetu wa ndege, kwa hiyo msiwe na wasiwasi” alisema Bw. Alphayo Kidata
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Dkt. Maduhu Kazi pamoja na kuipongeza Serikali Mkoani humo kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ambayo inasaidia kurahisisha uwekezaji alitoa wito kuendelea kuhamasisha uwekezaji pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli hiyo.
“Naomba tu niwapongeze Serikali Mkoani hapa, kazi ya kuvutia uwekezaji mnayoifanya ni njema, sisi tunawaunga mkono na pia msisite kuwaleta TIC pale wanapoonekana kuwa na changamoto” alisema Dkt Kazi.
Nae Mkuu wa Wilaya Mtwara Bw. Dunstan Kyobya alisema milango ya uwekezaji katika sekta zote ipo wazi katika Wilaya yake ambayo imekuwa ikipokea wageni wengi kuliko maeneo mengine ya mikoa ya Kanda ya Kusini.