……………………………………………………………….
RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni ametangaza Jumamosi ya wiki hii kuwa siku ya kitaifa ya maombi kwa ajili ya Covid-19.
Rais huyo amesema kuwa alipata wazo kutoka kwa raia wa Uganda ambaye alipata na “maono kutoka kwa Mungu.”
Kupitia ujumbe wake wa mtandao wa kijamii, Rais Museveni ameandika: “Mungu alikuwa amemuambia katika maono kwamba ninapaswa kuandaa maombi, yaandaliwe kisayansi, ili Mungu atuponye na Covid-19.
“Ninatangaza tarehe 29 Agosti, 2020, siku ya maombi ya kitaifa na siku ya mapumziko ya umma. Kaeni majumbani mwenu au kwenye viwanja vya nyumba zenu na muombe,” amesema Museveni.
Hadi sasa Uganda imerekodi watu 2,679 wenye maambukizi ya virusi vya corona na vifo 28.
Serikali iliweka masharti ya kudhibiti maambukizi hayo baada ya kuthibitisha kisa cha kwanza mwezi Machi mwaka huu.