………………………………………………………………
NA DENIS MLOWE,IRINGA
MSANII wa muziki wa bongo fleva anayekuja kwa kasi kutoka Nyanda za Juu Kusini mwenye makazi yake mkoani Iringa, Ezra Msiliova ‘ Eze Nice’ ametoa IP yenye nyimbo tano ikiwa kama zawadi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kazi alizofanya kwa kipindi cha miaka mitano.
Kuelekea kwenye michakato ya uchaguzi msanii huyo alisema kuwa nyimbo zilizoko katika IP hiyo zimeelezea kazi nzuri alizofanya Rais Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano tangu achaguliwe na nyingine ikiwa wimbo wa kumsifu mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Mnec Salim Abri ‘ Asas’ kwa mengi aliyofanya katika mkoa wa Iringa
Akizungumza na wanahabari, Eze Nice alisema kuwa nyimbo hizo tano ambazo ni zawadi tosha kwa Rais John Magufuli, makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Iringa, Salim Abri ‘Asas’ kwani amezipa majina Magufuli na Asas ikiwa ni vile ambavyo wameweza kufanya makubwa kwa maendeleo ya nchi na mkoa wa Iringa kwa ujumla.
Eze Nice ambaye amejichukulia maarufu mkoani Iringa kwa kuwa na nyimbo mbalimbali za kuhamasisha maendeleo na nyingine nyimbo za siasa amekuwa msanii wa kwanza kutoka mkoani hapa kuweza kuimba wimbo wa kumsifia Magufuli, Makamu wa Rais Samia na Salim Abri kwa kuona wanastahili sifa hivyo kutoa zawadi za nyimbo hizo kwao.
Alisema kuwa wimbo huo wa kwanza unajulikana kwa jina la Magufuli ambao ameelezea kwa undani kazi zilifanywa na Rais kwa kipindi hiki na wimbo wa pili ni zawadi kwa Salim Abri ambaye amekuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa mkoa wa Iringa hivyo ili kuwaenzi kwao ametunga nyimbo hizo wimbo wa tatu kwenye IP hiyo unaitwa Iringa ya Sasa ambao umeelezea mabadiliko ya maendeleo yaliyoletwa katika awamu ya tano.
Akielezea wimbo wa nne alisema kuwa umeupa jina la Mama Samia ukiwa na maudhui ya kumsifia makamu wa Rais kwa kazi nzuri anayofanya kwa kushirikiana na Rais John Maguguli hali ambayo unaona kabisa ukimpa nafasi mwanamke maendeleo yanaonekana kwa haraka Zaidi.
Alisema kuwa nyimbo hizo ambazo zimefanywa chini ya mzalishaji yeye mwenyewe kwenye studio New Record ya mjini Iringa zinatarajia kuwa kali kwani ziko katika mahadhi ya rumba na nzuri kwa ajili ya kucheza na kusikiliza ujumbe uliotolewa.
“Mwandishi nikwambie kitu hawa watu wamefanya makubwa sana kwa Tanzania na mkoa wa wetu Rais wetu kafanya yake Tanzania na kwa upande wa Mnec Salim Asas kwa mkoa wa Iringa kafanya mengi sana kwa kweli na vitu alivyofanya hadi sasa ni vingi sana sina cha kumpa Zaidi ya wimbo huu ambao umeelezea mengi aliyofanya kwa mkoa wetu hivyo zawadi hii nawapa wao kila mmoja kwa kuwa na wimbo wake,” alisema
Alisema kuwa nyimbo zote zinafanyiwa video na Shama Kilasi ambaye amekuwa akifanya video za wasanii wengi wa Nyanda za Juu Kusini na anatarajia baada ya wiki mbili au tatu zitatoka na watu waweze kuziona ubora wake na ujumbe uliomo kwenye nyimbo hizo.
Aidha Eze Nice alivishukuru vyombo vya habari kwa kuweza kumsimamia katika kazi zake zinaonekane kwa kuzipiga au kumtolea habari zake na kutoa wito kwa wasanii wengine kutokata tamaa kwa kuwa Sanaa yoyote inahitaji sana nidhamu, heshima na uvumilivu ili kuweza fikia malengo.
Alisema kuwa malengo yake kuwa msanii mkubwa ambaye ataleta mabadiliko makubwa katika Sanaa ya muziki akiwa chini ya kampuni hiyo kwa kuwa malengo yapo na nia anayo katika kufikisha muziki mbali Zaidi kuliko ilivyo sasa.
Alisema kuwa amejipanga vyema kuweza kukabiliana na changamoto zilizoko katika Sanaa ya muziki wa bongo fleva akiwemo baadhi ya radio kuchagua wasanii na kuacha kucheza nyimbo nzuri za wasanii wanaibuka miaka ya hivi karibuni.