Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa akimtwisha mama ndoo ya maji alipotembelea mradi wa maji wa Mwawaza-Negezi Manispaa ya Shinyanga.
Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Negezi alipotembelea mradi wa maji wa Mwawaza-Negezi Manispaa ya Shinyanga.
Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa akikagua nyaraka za ujenzi wa mradi wa maji wa Ngogwa-Kitwana.
Tanki la maji la lenye ujazo wa lita 680,000 lililojengwa katika katika Kijiji cha Ngogwa na wataalamu wa ndani kupitia ‘force account’.
………………………………………………………………….
Na Evaristy Masuha.
Mwezi Agosti 2020 Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) alifanya ziara ya kikazi mkoani Shinyanga ambapo alikagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji.
Moja ya watu waliompokea Prof. Mbarawa ni Mzee Renatus Myovela, mtumishi mstaafu, anayeishi katika Kijiji cha Ngogwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Mzee Myovela amesema aliitumikia sekta ya maji kwa takriban miaka 40, kuanzia mwaka 1970.
Mzee Myovela amesema kuwa baada ya utumishi wake alirudi Wilayani Kahama kuendelea maisha ya ustaafu. Akiwa huko wataalam wa Wizara ya Maji waliamua kumpa jukumu la kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Tanki la maji la Ngogwa ambalo ujazo wake ni Lita 680,000.
Tanki hili liko katika mradi wa maji wa Ngogwa-Kitwana ambao unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.4 na ukitarajia kuwanufaisha wananchi wapatao 20,095.
Mzee Myovela, akiongea mbele ya Prof. Mbarawa kuhusu utaratibu wa kuwatumia wataalam wa ndani katika utekelezaji wa miradi, anasema kwamba ndani ya miaka 40 ya utumishi wa Umma hakuwahi kushuhudia mradi mkubwa kama huo ukitekelezwa na wataalamu wa Wizara kupitia utaratibu wa ‘force account’. Anasema nyingi ya kazi hizo zilifanywa kupitia Wakandarasi.
Mzee Myovela alisema kuwa utaratibu huo ni mzuri na kwamba uendelee kwani unawapa uzoefu wataalamu mbalimbali katika sekta ya maji.
Ameongeza kuwa Tanzania inao Wahandisi wengi kwa sasa, hivyo ni muhimu watumike katika utekelezaji wa miradi ya maji.
“Inawezekana kulikuwa na hali ya kutojiamini kwa wataalam kwani muda mwingi tuliutumia kusimamia badala ya kutekeleza sisi wenyewe. Hii ilikuwa ikisababisha mara nyingi kukimbizana na Wakandarasi kuwataka waharakishe utekelezaji wa miradi jambo ambalo sikuliona wakati wa utekelezaji wa mradi huu”, Mzee Myovela amesema.
Ameongeza kuwa anayo mengi ya kujifunza hasa katika utekelezaji wa miradi ya maji kwa kutumia utaratibu wa ‘Force Account’ ambao unawatumia zaidi watalaam wa ndani badala ya wakandarasi katika utekelezaji wa mradi.
Waziri wa Maji Mhe. Profesa Mbarawa (Mb) anasema tangu kuanza kwa utaratibu huo, matokeo makubwa yameonekana na anawataka wataalam wa Wizara yake kujiandaa kutekeleza miradi mbalimbali kwa mtindo huo.
Prof. Mbarawa anasema baada ya kuanza kutumia utaratibu huo Serikali imeweza kukamilisha miradi kwa haraka zaidi, gharama za utekelezaji wa miradi zimepungua kwa kiasi kikubwa na umesaidia kuondoa migongano baina ya Serikali na wakandarasi.
Pia, umesaidia kutekeleza miradi kwa kutumia vifaa ambavyo vina ubora stahili, vinavyoagizwa moja kwa moja kutoka viwandani, ukilinganisha na vifaa ambavyo vimekuwa vikitumika na baadhi ya wakandarasi wasio waaminifu.
Ipo mifano michache iliyodhihirika katika ziara hiyo. Mradi wa maji wa Ngogwa-Kitwana ulipangwa kutekelezwa na mkandarasi kwa shilingi bilioni 4.6.
Baada ya kuamua kuwakabidhi wataalamu wa wizara, mradi huo unatarajiwa kukamilika kwa shilingi Bilioni 2.4 gharama ambayo ni nusu ya gharama ambazo zingetumika kama mradi ungekabidhiwa kwa mkandarasi.
Mradi huo ulioanza kutekelezwa mwishoni mwa mwezi Machi 2020 unatarajia kukamilika ndani ya miezi sita jambo ambalo linatajwa na Waziri Prof. Mbarawa kuwa ni muda mfupi sana ukilinganisha na muda ambao wakandarasi wamekuwa wakiutumia kutekeleza miradi ya aina hiyo.
Mradi mwingine ni ule wa Mwawaza-Negezi unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA)ambao unawanufaisha wakazi wapatao 6,417. Mradi huo ulipangwa kutekelezwa kwa shilingi bilioni 2 iwapo ungekabidhiwa kwa mkandarasi.
Baada ya kuamua kutekelezwa na wataalamu wa wizara unatarajiwa kutumia shilingi Bilioni 1.4 na utakamilika ndani ya kipindi cha chini ya miezi sita.
Faida nyingine kubwa ya matumizi ya utaratibu huu ni kuwa unawafanya wahandisi wa wizara kushiriki moja kwa moja kwa vitendo kile walichosomea.
Pia, unawapa nafasi na muda wa kutosha wataalamu kwa kuyaweka katika utekelezaji maarifa waliyosomea na kupata ya ziada ambayo hawakuwa nayo.
Vilevile, usimamizi wa miradi ya aina hii inakuwa nafuu zaidi kwani inahusisha wataalamu ambao ni waajiriwa wa Wizara tofauti na mkandarasi ambaye anaweza kuhamia sehemu nyingine. Hivyo, ili kumpata inabidi kutafutwa.
Profesa Mbarawa anasema baada ya kushuhudia mafanikio makubwa ya utaratibu huu, anawataka wataalamu wa Wizara kujiandaa kuanza kutekelezamiradi yote ya maji kwa utaratibu wa force account.
Anawataka wajiamini kwani wamesoma na kuelimika.
“Ndoto yangu sasa ni kuhakikisha miradi yote ya maji inatekelezwa na wataalamu wetu” Prof. Mbarawa anasema.
Waziri anawapongeza wataalam wa sekta ya maji kwa kufanikiwa kujenga matenki makubwa likiwemo la Morogoro ambalo ujazo wake ni lita milioni mbili.
Anasema ndoto yake sasa ni kujenga tenki lenye ujazo wa lita milioni sita ambalo limepangwa kujengwa wilayani Tandahimba mkoani Mtwara.
Anasema baada ya hapo wataalamu wa sekta ya maji waliosoma na wakabobea wataanza kujenga mfumo wa kutibu maji (water treatment plant) kwa mfano wa ule uliojengwa Ihelele Misungwi mkoani mwanza ambao majiyake yanasafirishwa katika mikoa ya Shinyanga na Tabora, Profesa Mbarawa anasema hakuna linaloshindana.
Tuipongeze Wizara na wadau wote waliowezesha haya yote ambayo yanaleta tija katika kutoa huduma kwa wananchi, pamoja na wataalam ambao kwa sasa wanayaishi maisha na kuyafanya yale waliyosomea. Huu ndio uthubutu.