Kamanda wa polisi mkoani Dodoma Gilles Muroto akizungumza na vyombo vya habari leo Ofisini kwake Jijini Dodoma Juu ya usalama wa wanadodoma kuelekea Kampeni za Uchaguzi Mkuu.
……………………………………….
Na.Majid Abdulkarim,Dodoma.
Kamanda wa polisi mkoani Dodoma Gilles Muroto amesema kuwa jeshi hilo limejipanga imara kukabiliana na wale wote watakaokuwa na nia ovu ya kufanya vurugu na kuhatarisha amani katika kampeni za vyama mbalimbali za siasa kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, 2020.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dodoma wakati kamanda huyo akizungumza na waandishi wa Habari .
Aidha Muroto amebainisha kuwa makundi yote ya ovyo ambayo yamejiandaa kwa ajili ya kuleta vurugu yatashughulikiwa na kazi ya jeshi la polisi ni kulinda amani ya Tanzania na maliza za watanzania.
Katika hatua nyingine Kamanda Muroto amesema kuwa jeshi la Polisi litahakikisha linafuatilia kwa makini mwenendo wa kampeni na kubainisha kuwa Tanzania haina Mjomba wala shangazi nje ya nchi huku akiwataka waandishi wa Habari kutumia kalamu zao vizuri kuhakikisha hakuna Habari za uchochezi.
Lakini pia Kamanda Muroto ametoa wito kwa watanzania kuacha watu wa kulinda nyumba pindi wanapokwenda kwenye shughuli mbalimbali ili pasitokee uhalifu wowote na jeshi la polisi litahakikisha lina linda usalama wa mali na wananchi wake.