Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Charles,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) usiku wa leo katika Ofisi za Tume zilizopo Njedengwa jijini Dodoma akitoa taarifa kwa umma kuhusu kuhusu kutupilia mbali mapingamizi yaliowasilishwa ya wagombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
……………………………………………
Na. Alex Sonna, Dodoma
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetupilia mbali mapingamizi yote yaliyokuwa yamewekwa na Mgombea wa Urais wa CHADEMA Tundu Lissu dhidi ya Mgombea wa urais wa CCM Dkt John Magufuli na Mgombea Urais wa CUF Ibrahim Lipumba ambapo tume hiyo imesema kuwa wagombea hao wamefuata taratibu zote za sheria ya uchaguzi na hakuna kasoro yoyote walioibaini katika mapingamizi hayo.
Kauli hiyo imetolewa usiku wa leo na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Charles wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ofisi za Tume zilizopo Njedengwa jijini Dodoma.
Dkt. Charles kuwa tume imetupilia mbali mapingamizi hayo baada ya kujiridhisha kwamba pingamizi hizo hazina msingi wa kisheria hivyo kufanya wagombea hao kubaki wagombea halali wa kiti cha Urais wa Uchaguzi mkuu utakaofanyika 28 Oktoba mwaka huu .
“Kwa msingi wa uamuzi huu vyama vya siasa vinavyo shiriki uchaguzi mkuu wa kiti cha urais na makamu wa rais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu vinabaki kuwa 15”, amesisitiza Dkt. Charles
Aidha Dkt. Charles amesema kuwa tume imepokea pingamizi kutoka kwa Mgombea Urais kupitia CHADEMA Tundu Lissu dhidi ya Prof. Ibrahim Lipumba mgombea urais CUF na Dkt. John Pombe Magufuli mgombea kwa tiketi ya CCM.
Dkt. Charles ameeleza kuwa tume kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 39 ya kanuni ndogo ya tano ya uchaguzi wa rais na wabunge za mwaka 2020 baada ya kupokea pingamizi dhidi ya wagombea hao tume imewataaifu wawekewa pingamizi mapema na wahusika kuwasilisha utetezi wao.
Pingamizi dhidi ya mgombea wa CUF ni kwamba hakurudisha fomu za uteuzi kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na kwa mujibu wa sheria.
Dkt. Charles amesema kuwa tume baada ya kupitia sababu za pingamizi pamoja na utetezi uliotolewa imejiridhisha kuwa Prof. Ibrahim Lipmba amerejesha fomu zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo ya tume ya taifa ya uchaguzi.
“Hivyo tume imejiridhisha kwamba pingamizi halina msingi wa kisheria na imetupiliwa mbali na kwa maana hiyo Prof. Lipumba anaendelea kuwa Mgombea halali wa kiti cha urais kupitia tiketi ya chama cha CUF”,ameeleza Dkt. Charles.
Pia Dkt. Charles ametoa ufafanuzi kuwa pingamizi dhidi ya Mgombea wa CCM , mleta pingamizi anadai kwamba mgombea urais kupitia CCM Dkt. John Pombe Magufuli hakuambatanisha picha kwenye fomu ya uteuzi na hakurudisha fomu ya uteuzi kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria.
“Tume baada ya kupitia sababu za pingamizi zote mbili kwa pamoja na utetezi uliotolewa imejiridhisha kuwa Dkt. John Pombe Magufuli mgombea urais kpitia CCM amerejesha fomu zake ambazo zimeambatishwa pamoja na picha kwa mujibu wa sheria kanuni na maelekezo ya tume”,amesema Dkt. Charles
Hivyo Dkt. Charles ameweka wazi kuwa tume imejiridhisha kwamba pingamizi hizo hazina msingi wa kisheria na kuzitupilia mbali.