Sehemu ya wana CCM waliojitokeza kumsindikiza kuchukua fomu za kugombea Urais Ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). |
Na Joachim Mushi, Zanzibar
MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Mwinyi leo ameisimamisha Zanzibar na viunga vyake alipojitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa nafasi ya urais wa Zanzibar katika Ofisi za Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Maisara.
Mgombea huyo ambaye tayari ameahidi neema ya ajira kwa vijana ikiwa ni utekelezaji wa sera ya chama hicho iliyowekwa mwaka 2020-2025 itakayoleta ajira takribani 300,000 kwa Vijana, amezindikizwa na mamia ya wanachama na vijana waliokuwa katika maandamano yake.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la Tume baada ya kukabidhiwa fomu yake na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud ameahidi kulisimamia suala hilo kipekee ili kupunguza kero ya ajira.
Dk Mwinyi alisema miongoni mwa vipaumbele vyake ambavyo vinatokana na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025, ni kuimarisha sekta ya viwanda, utalii na uvuvi wa bahari kuu kwa ajili ya kuzalisha nafasi za ajira, ambapo amekusudia kutekeleza sera na ilani ya chama hicho kwa vitendo kama watangulizi wake.
“Mimi kama mgombea wa Chama Cha Mapinduzi nitainadi ilani hiyo ya ajira 300,000 lakini lazima vijana tuwaandae tuwape mafunzo tuwe na vyuo vya utalii, vyuo vya uvuvi ili vijana wawe weledi, nataka niwaambie vijana wakae tayari kuingia katika soko la ajira wawe tayari kufanya kazi,”
Alibainisha kuwa tayari mikakati imewekwa katika kuwaandaa Vijana kuingia katika soko la ajira kwa kuimarisha Vyuo vya utalii, pamoja na Uvuvi ambavyo vitawaandaa Vijana kuweza kuvua katika uvuvi wa bahari kuu.
“Natambua kuna changamoto nyingi zinazowakabili vijana lakini lazima tukuze uchumi, lazima tuwe na sekta za vipaumbele ukitizama eneo la utalii, suala la uvuvi, suala la viwanda hayo maeneo tukiyafanyia kazi sina shaka tutaongea idadi ya uajira kwa vijana wetu,”
Aidha akizungumzia kuhusu kukuza uchumi, alibainisha kuwa hatokuwa tayari kuachia rushwa ifanyike chini ya utawala wake na wale wote ambao wana tabia ya kukwepa kodi basi wajue kwamba hawatopata nafasi chini ya serikali yake ambayo amekusudia kuiongoza iwapo atapata ridhaa ya kuongoza katika kipindi chake.
Pamoja na hayo aliwataka wapinzani wa CCM kutambua kuwa chama hicho hakijagawanyika baada ya kumalizika kwa mchakato wa kura za maoni, bali kipo vizuri kiushirikiano na wagombea wote walioshiriki katika mchakato wa awali.
”Viongozi wenzangu katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu nawaomba tusubiri wakati ufike tutafanya kampeni za kistaarabu sana zenye amani na utulivu kauli ambazo zitakuwa na lengo la kuwaunganisha wananchi na sio kuwagawa kwa kuwabaguwa ”alisema mgombea huyo.
Awali akimkabidhi fomu ya ugombea, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Mkuu mstaafu Mahmoud alimueleza mgombea huyo masharti yanayopaswa kufuatwa yalioandikwa kwenye fomu hizo.
“Ili mtu ateuliwe na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwa mgombea nafasi ya urais awe na sifa ya kugombea, achukue na kujaza na kurejesha fomu ya uteuzi iliyotayarishwa na tume ya uchaguzi kabla ya muda uliowekwa Tume, na fomu ya uteuzi iliyojazwa na mgombea iwasilishwe pamoja na maelezo binafsi ya mgombea kama inavyohitajika kutolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa pamoja kuwasilishwa hati ya kiapo katika muda uliwekwa iliyojazwa na kutiwa saini za wadhamini wa mikoa yote ya Zanzibar pamoja na picha nne zilizopigwa miezi mitatu nyuma kabla ya uteuzi,” alisema Mwenyekiti wa ZEC. Jaji Mkuu MstaafuHamid Mahmoud.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Abdalla Juma Sadalla (Maabodi) aliwataka wanachama na wafuasi wote wa chama cha Mapinduzi kuhakikisha wanajitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 ili kukipa ushindi chama hicho kwani bila ya kupigwa kura kwa wingi hakuna ushindi.
”Nikwambieni hivi njia pekee ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka 2020 ni kwa wanachama na wafuasi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura mgombea wetu Dk Hussein Mwinyi na kumfanya kuwa rais wa Zanzibar, kwa hivyo siku ikifika mjitokeze kwa wingi sana kwenda kumpigia kura yeye na wabunge wetu na wawakilishi pamoja na madiwani,” alisema Naibu huyo.