*************************
Na John Walter-Manyara
Wafanyabishara mkoani Manyara wametakiwa kutumia fursa ya michezo katika kuutangaza mkoa wa Manyara na biashara zao.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti leo Agosti 24,2020, wakati akizungumza na wafanyabiashara mkoani hapo katika kikao kilichofanyika mjini Babati.
Aidha Mkirikiti ameitaka Halmashauri ya mji wa Babati, iharakishe ujenzi wa uwanja wa Michezo Kwaraa unaoendelea kujengwa kwa sasa kwa vibanda vya biashara kuzunguka uwanja huo.
Amesema kukamilika kwa uwanja huo utafungua fursa ya shughuli za kimichezo na burudani mbalimbali kufanyika katika uwanja huo jambo ambalo litaongeza ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya mji na mkoa kwa ujumla.
Kwa upande mwingine amelitaka Shirika la Umeme mkoani humo kuhakikisha wanauwaunganishia umeme wananchi pindi wanapohitaji na kuondoa utiritimba uliopo ili wananchi waendelee kutumia nishati hiyo katika biashara zao.
Mwenyekiti chama cha wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Manyara Stanley Mchome, amesema Wanaridhishwa na utendaji wa awamu ya tano huku akiomba ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali uendelee.