Na John Walter-Babati
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti ameiagiza idara ya Ardhi Halmashauri ya Mji wa Babati kuweka ratiba ya kusikiliza kero za wananchi na kutatua migogoro ya ardhi iliopo.
Amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kwa kiwango kikubwa kujua chanzo cha migogoro hiyo na kuipatia ufumbuzi wa haraka.
Mkirikiti ametoa agizo hilo baada ya kupokea kero nyingi zinazohusu ardhi wakati alipofanya mkutano na wananchi mjini hapo leo Agosti 24,2020.
Kwa upande mwingine amewataka wananchi wote waliowasilisha malalamiko na wenye kero kufika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Babati agosti 28 mwaka huu kwa ajili ya ufumbuzi wa malalamiko na kero zao.
Hii ilikuwa ni ziara yake ya kwanza mjini Babati tangu aanze kuwatumikia wananchi hao mapema mwezi Julai akimpokea mtangulizi wake Alexender Mnyeti aliekwenda kugombea Ubunge jimbo la Misungwi mkoani Mwanza kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi.
Mapema Mkuu wa mkoa alizungumza na wafanyabiashara mkoani hapo na kusikiliza kero zinazowakabili hukuvakiwaahidi ushirikiano.