Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt. Maduhu Isaac Kazi (Kulia) akijadiliana jambo na Mwakilishi wa Kampuni ya Elsewedy ya Misri Injinia Ibrahim Qamar mapema Juzi katika Ofisi za TIC zilizopo Mtaa wa Shaban Robert Posta Jijini Sar Es Salaam, katikati ni Mkuu wa Idara ya Uwezeshaji kwa Wawekezaji Bw. Revocatus Arbogast Rasheli akifuatilia kwa makini mjadala huo.
Mrugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Dkt. Maduhu Isaac Kazi (Mwenye Tai Nyekundu Kulia) akiwa katika Picha ya Pamoja na Injinia Ibrahim Qamar, Mwakilishi Mwekezaji wa Kampuni ya Elsewedy ya Misri anaewekeza Nchini kwa kujenga Kiwanda cha Vifaa vya umeme na Chuo cha fani ya Umeme.
*************************************
Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Mwakilishi wa Kampuni ya kuzalisha vifaa vya umeme ya Elsewedy Electric ambaye ni Mkurugenzi Mkaazi wa Afrika Mashariki wa Kampuni hiyo injinia Ibrahim Qamar kutoka nchini Misri anayewekeza nchini Tanzania amesema kuimarika kwa Sera, Sheria na mazingira mazuri ya Uwekezaji Nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na amani na utulivu; ndio sababu kubwa zilizomfanya aje kuwekeza nchini.
Bw. Qamar amesema miongoni mwa masuala ambayo wawekezaji wengi huyaangalia kwa makini kwenye nchi wanazotaka kuwekeza ni pamoja na Utawala bora, ulinzi wa mitaji yao pamoja na masoko ya uhakika mambo ambayo Tanzania imeyapa kipaumbele na hivyo kumfanya yeye na wawekezaji wengine kufikiria na kuamua kuwekeza Tanzania
Bw. Qamar alitembelea ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC mwishoni mwa juma lililopita na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho Dkt. Maduhu Kazi ambapo alimwambia kutokana na kazi nzuri wanayoifanya, ameamua kuwekeza katika miradi miwili mikubwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha kutengeneza vifaa vya Umeme pamoja na Chuo cha mafunzo ya umeme, uwekezaji ambao unatarajia kufanyika kwa awamu mbili na baadae huenda atafanya uwekezaji katika viwanda vya kutengeneza vifaa na kujenga miundombinu ya kuzalisha umeme wa jua na upepo.
Awamu ya kwanza ya uwekezaji huu ambao unapanga kuwekeza mtaji wa Dola za Marekani milioni kumi na tano (15) na kuzalisha ajira za moja kwa moja mia moja kumi na tano (115) unatarajia kuanza mara moja baada ya taratibu za ardhi kukamilika katika wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es salaam. Mwekezaji huyu pia aliishukuru TIC kwa jitihada za kuhakikisha inasimamia upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji huo ambao utakuwa na tija kubwa kwa Taifa na Jamii ya Tanzania. “TIC mnafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wawekezaji tunapata fursa ya kuwekeza hapa Tanzania, mmetusaidia sana kupata ardhi kule kigamboni ambayo tulikuwa tukiihitaji kwa muda mrefu na kulikuwa na ucheleweshaji katika hatua za kuipata, lakini niseme tu, baada ya TIC kuingilia kati suala hili, nimeona mafanikio makubwa sana na nawaahidi sitawaangusha katika uwekezaji huu mkubwa ambao najua utakuwa na manufaa kwa pande zote mbili. Nakusudia kujenga kiwanda cha vifaa vya umeme vikiwepo Mita, Waya na Transifoma, pia tutafungua chuo cha masuala hayo nikutaarifu tu kuwa awamu ya kwanza tutaianza mara moja, pale taratibu za kupata ardhi zitakapokamilika ambapo naona tupo katika hatua za mwisho kabisa na mimi nimeshajipanga vizuri kabisa ili niweze kuanza” alisema Bw. Qamar.
Pia alimshumshukuru Mkrugenzi Mtendaji wa TIC Dk. Maduhu Kazi kwa kutembelea ofisi za kampuni ya Elsewedy Electric Jijini Dar es Salaam muda kifupi baada ya kuteuliwa kuiongoza taasisi hiyo ya Uwekezaji nchini ambapo alipata fursa ya kujua mpango wa kampuni wa uwekezaji pamoja na changamoto zilizokuwa zinaukabili uwekezaji huo hivyo kukwamisha uwekezaji wa kampuni hiyo nchini ambapo katika ziara hiyo TIC ilimhakikishia mwekezaji Elsewedy kuwa TIC ingeshughulikia changamoto hizo kwa kasi sambamba na miradi mingine ambayo uwekezaji wake ulikwama kwa sababu za kiutendaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt Maduhu Kazi amesema Kituo hicho kinahudumia wawekezaji wote na kwamba endapo kuna changamoto zozote wanazokutana nazo wasisite kuziwasilisha katika ofisi za TIC zilizopo katika kanda na hata hapa makao Makuu. Aidha Dkt. Kazi amesema jitihada alizozifanya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli katika kuboresha mazingira ya Uwekezaji na Biashara yamesaidia wawekezaji wengi kuiamini Tanzania kama nchi salama kwa kuwekeza mitaji yao. “Milango ya TIC ipo wazi wakati wote, tunawakaribisha sana na endapo mna changamoto zozote msisite kuja, hii ni kazi yetu” alisema Dkt Kazi. Aidha aliwataka wawekezaji wengine kuja kuwekeza nchini kutokana na kuimarika kwa Sera na sheria za Uwekezaji zilizofanywa na Serikali ya awamu ya tano hatua inayoleta manufaa makubwa kwenye sekta ya uwekezaji nchini na kuwezesha kufikiwa kwa azma ya Taifa ya kujenga uchumi wa viwanda kama ilivyobainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025. Aidha alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia Oktoba 2015 hadi sasa Serikali imefuta kodi na tozo mbalimbali 168 ambazo zilikuwa kero kwa wawekezaji na pia katika kipindi hicho hakuna kodi yoyote mpya iliyoanzishwa na Serikali hatua inayoendelea kuipaisha Tanzania katika kuvutia Uwekezaji.