Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya Utumishi wa Umma Kapt Mstaafu George Mkuchika kulia akiondoa kitambaa kama ishara ya uzinduzi na ufunguzi rasmi ya ofisi ya Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Takukuru wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma jana,kushoto anayeshuhudia Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Kapt Mstaafu George Mkuchika wa nne kushoto akikata utepe kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa jengo jipya la Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(TAKUKURU)wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,wa tatu kushoto mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme,kushoto kwa Waziri Mkuchika mkurugenzi wa kuzuia Rushwa Sabina Seja na wa tatu kulia kaimu mkuu wa wilaya ya Namtumbo Pololet Mgema,
Picha na Muhidin Amri
……………………………………………………
Na Muhidin Amri,
Namtumbo
WAZIRI wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na utawala bora Kapten mstaafu George Mkuchika,amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri na wakuu wa wilaya hapa nchini kutoa majengo kwa ajili ya matumizi ya ofisi za taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Takukuru pale ambapo taasisi hiyo haina majengo.
Waziri Mkuchika ametoa agizo hilo jana wakati akizindua jengo la taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma na kusisitiza kuwa, ni haki kwa Takukuru kutumia majengo ya Serikali pale inapokosa ofisi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.
Alisema, kuna majengo yasiozidi thelathini kati ya mahitaji ya majengo zaidi ya mia moja nchini ,kwa hiyo pale taasisi hiyo inapokosa ofisi ni wajibu wa viongozi wa eneo husika kutoa majengo ya serikali yaliyopo ili yatumiwe na Takukuru.
“nisije kusikia eti wilaya fulani takukuru imekosa majengo ya kufanyia kazi, jambo hilo sitokubaliana nalo hata kidogo,ni wajibu wa viongozi kutafuta na kutoa majengo kwa takukuru pale ambapo Serikali haijajenga majengo ya Takukuru”alisema Mkuchika.
Aidha, amewataka wananchi wa Namtumbo kuitumia vizuri ofisi ya Takukuru ili kwa pamoja washiriki kuijenga wilaya hiyo na Tanzania kwa jumla kwa kuzuia na kupambana na Rushwa sambamba na kuwafichua wala rushwa na waache kushiriki vitendo vya rushwa ili kufikia maendeleo.
Alisema,Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuri imefanya kazi kubwa kuimarisha na kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi hapa nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuchika mapambano dhidi ya rushwa yanayofanywa na Serikali ya awamu ya tano imesaidia kuharakisha maendeleo na kukua kwa uchumi ambapo ripoti ya Benki ya Dunia ya Septemba mwaka jana, imeitaja Tanzania imeongoza kupunguza umaskini miongoni mwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.
Pia alisema, ripoti nyingine ya Benki ya Dunia inayoitwa(Human Capital the Real Wealth of Nations ya Julai 2019 ilionesha umaskini nchi I Tanzania umepungua kutoka asilimia 34.4 hadi kufikia asilimia 26.8.
Alisema, ufanisi wa jitihada za Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa nchini kwa mwaka 2018/2019 zimeendelea kuonekana kupitia taarifa za utafiti wa kupima hali ya rushwa Duniani unaofanywa na wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora.
Mkuchika alisema, kufunguliwa kwa ofisi ya Takukuru wilayani Namtumbo ni ushahidi tosha na namna gani Serikali ya awamu ya tano ilivyodhamiria kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuijengea uwezo zaidi kiutendaji taasisi hiyo.
Ameitaka Takukuru kuhakikisha wananchi wanapata haki wanazostahili popote wanapokwenda kupata huduma na pale wanaponyang’anywa na mtu au taasisi yoyote kwa njia za rushwa.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme, ameipongeza Takukuru kwa kazi nzuri inayofanya katika kuzuia na kupambana na watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa hapa nchini.
Alisema, jengo hilo ni muhimu sana katika kuimarisha utendaji kazi kwa watumishi wa Takukuru watakaopangiwa kufanya kazi katika wilaya ya Namtumbo na litawarahisishia watoa taarifa pamoja na mashahidi watakaoletwa katika operesheni mbalimbali kuwa na uhuru na usiri mkubwa.
Naye kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Sabina Seja alisema,hadi kufikia mwezi julai mwaka huu Takukuru imejenga jumla ya ofisi za mikoa 28 na ofisi katika wilaya 117,lakini kati ya ofisi hizo majengo yanayomilikiwa na Takukuru ni 22 kwa ngazi ya mikoa na majengo 22 katika wilaya.
Kwa mujibu Seja ambaye ni mkurugenzi wa Uzuiaji rushwa alisema, kwa sasa kuna upungufu wa majengo 6 ya mikoa na 95 ngazi ya wilaya hivyo matumaini ya Taasisi hiyo kwamba Serikali itaendelea kuipatia fedha ili iweze kukamilisha ujenzi katika mikoa na wilaya.
Amewashukuru wadau wa mapambano dhidi ya rushwa katika mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa mkoa Christina Mndeme, kutokana na ushirikiano ambapo hadi kufikia juni 2020 Takukuru Ruvuma imeweza kufanya kazi kubwa ya kuchunguza ubadhirifu na kuweza kuokoa kiasi cha shilingi 740,799.861.
Seja alisema kuwa,fedha hizo zimeokolewa kutokana na uchunguzi katika benki ya wananchi Mbinga,vyama vya ushirika(Amcos) na Saccos na baadhi ya watuhumiwa wa ubadhirifu kurejesha fedha.
Alisema, vitendo vya vilikuwa vinadumaza maendeleo ya ushirika nchini hivyo wanaamini kuwa kwa hatua hiyo Takukuru italeta mabadiliko katika uendeshaji wa ushirika nchini.