Nyumba za walimu (sita katika moja) zilizopo katika shule ya Sekondari ya kutwa ya Sawe iliyopo katika Kijiji cha Saawe, Kata ya Masama Mashariki, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
(Picha na Daud Manongi – MAELEZO)
……………………………………………………………………….
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
SERIKALI imekusudia kuleta mapinduzi ya kiuchumi ili kuibadili Tanzania kuwa nchi ya
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Sekta ya elimu na mafunzo, kwa mujibu wa Dira
ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mpango wa muda mrefu wa Maendeleo ya Taifa
2011/12 hadi 2024/25, inatarajiwa kuleta maendeleo ya haraka ya rasilimali watu kwa
kutayarisha idadi ya kutosha ya Watanzania walioelimika na kupenda kujielimisha
zaidi ili kulifanya Taifa lipate maendeleo na kuwa lenye uchumi wa kati na shindani
ifikapo mwaka 2025.
Serikali iliandaa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ili kutoa mwelekeo
wa elimu na mafunzo nchini kwa kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi
na kiteknolojia na changamoto za elimu na mafunzo kitaifa, kikanda na kimataifa, ili
kuongeza fursa, ufanisi na ubora wa elimu na mafunzo nchini na kufikia viwango vya
rasilimaliwatu kwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Sera hii imeweka Dira ya elimu na mafunzo nchini kuwa ni “Mtanzania aliyeelimika na
mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia
katika kuleta maendeleo ya Taifa” na Dhima yetu kuwa ni “kuinua ubora wa elimu na
mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya
Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia
katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa letu”.
Akifungua rasmi Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma,
Novemba 20, 2015, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
magufuli pamoja na mambo mengine alisema, juhudi kubwa zimefanyika katika
upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu.
Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu
inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi. Aidha,
Serikali itahakikisha kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni
pamoja na maabara, vitabu, madawati, n.k.
Aliweka bayana kwamba Serikali itahakikisha kuanzia Januari 2016 elimu kuanzia
darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure. “Tutahakikisha kwamba
wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati. Tutashughulikia
maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za
walimu vijijini” alisema Rais Magufuli.
Akizungumza mwezi Juni mwaka huu, jijini Dodoma, wakati akifungua Mkutano Mkuu
wa Uchaguzi wa Chama cha Walimu (CWT), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa moja ya vipaumbele vya Serikali yake ni
kukuza na kuimarisha Sekta ya elimu nchini, na kuwa Serikali itaiendeleza sekta hiyo
hususan katika kupanua wigo na kuboresha elimu inayotolewa kuanzia ngazi ya awali
hadi elimu ya juu, sambamba na kuendelea kuajiri walimu .
Ni dhahiri shahiri kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutekeleza sera hiyo
ya elimu nchini kwa kufanya mapinduzi yanayolenga kuzalisha wasomi na watendaji
watakao iendeleza Tanzania ya viwanda na nchi yenye uchumi ulioimarika zaidi.
Mapinduzi hayo yanajidhihirisha katika maboresho ya sekta hiyo ambapo shule ya
Sekondari ya kutwa iliyopo katika Kijiji cha Saawe, Kata ya Masama Mashariki, Wilaya
ya Hai mkoani Kilimanjaro imenufaika kupitia utekelezaji unaofanywa na Serikali wa
kuboresha nyumba za walimu ikiwa ni sehemu ya kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Mradi wa ujenzi wa nyumba za walimu sita ndani ya moja (six in one) katika Shule ya
Sekondari Sawe yenye jumla ya wanafunzi 213 unatajwa kuboresha mazingira ya
kuishi walimu na kuongeza ufanisi wa kazi ya kufundishia.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Sawe, Gaudence Silayo anasema kuwa shule
hiyo ilipoanza mwaka 2007 haikuwa na nyumba za walimu, badala yake walimu
waliishi mitaani katika nyumba za kupanga na kutokana na hali ya hewa iliyopo katika
eneo hilo ya mvua nyingi na matope walimu walipata shida na walifika shuleni kwa
kuchelewa jambo ambalo lilishusha kwa kiwango kikubwa ufaulu wa shule hiyo.
“Mradi huu wa ujenzi wa nyumba sita katika moja ulipokuja kwa bajeti ya mwaka
2015/2016 wenye gharama ya shilingi 150,586,100 ambao ulikamilika mwaka 2017,
basi kuanzia wakati huo walimu sita waliweza kuishi hapa shuleni, jambo hilo lilileta
faraja na matumaini makubwa na liliongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa walimu”
anasema Mwalimu Silayo
Aidha, akifafanua faida za kuwepo kwa nyumba hizo, mwalimu Silayo anasema kuwa
shule iliandaa masomo ya ziada baada ya masomo ya darasani ambapo wanafunzi
walifaulu vizuri, kidato cha pili walifaulu wote isipokuwa mwanafunzi mmoja na
wanafunzi wa kidato cha nne walifaulu wote isipokuwa wanafunzi watatu.
Naye, mwalimu Germana Mtenga anayefundisha katika shule hiyo anasema kuwa faida
ya kuwa na nyumba zinatoa fursa kwa walimu kutoa msaada wa masomo wa ziada kwa
kwa wanafunzi hasa kwa sababu tayari walimu wamekuwa na utulivu, sambamba na
kuwasaidia wanafunzi wa kike wanapokuwa wamepata matatizo mbalimbali.
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imejipambanua
kuboresha sekta ya elimu nchini kwa kutoa elimu bila malipo katika shule za msingi
na sekondari, tangu Disemba, 2015 hadi Februari, 2020 imetumia jumla ya shilingi
Trilioni 1.01/=. Maboresho mengine ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule za
Msingi kutoka 16,899 zilizokuwepo mwaka 2015 hadi shule 17,804 mwaka 2020. Shule
za Sekondari nazo zimeongezeka kutoka 4,708 hadi 5,330 mwaka 2020.
Fauku ya hayo, ukarabati wa shule kongwe za Sekondari 73 kati ya shule Kongwe 89,
kujengwa mabweni 253 na nyumba za walimu na maabara 227, Serikali imetoa vifaa
vya maabara vipatavyo 2,956 na kupunguza tatizo la uhaba wa madawati kutoka
madawati 3,024,311 mwaka 2015 hadi madawati 8,095,207 mwaka 2020.
Vilevile bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu imeongezeka kutoka shilingi
bilioni 341 kwa mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi bilioni 450 mwaka 2019/2020.