Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo ( Bara) Bw. Gerald Kusaya akionyesha funguo za gari wakati alipokabidhi gari hilo pamoja na pikipiki mbili kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi Zanzibar Bi.Maryam Abdulla ( kulia) leo mjini Zanzibar.Gari hilo limetolewa kwa ajili ya uratibu wa Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu upande wa Zanzibar.
…………………………………………………………..
Serikali imesema itaendelea kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa kwa pamoja na Wizara ya Kilimo ya Zanzibar inakuwa na ubora na inakamilika kwa wakati ili kuwanufaisha wakulima nchini.
Kauli hiyo imetolewa mjini Zanzibar na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (Bara) Gerald Kusaya alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu nchini (TANIPAC) pamoja na mradi wa Kuimarisha Uzalishaji wa Mpunga (ERPP).
“Tunataka kuona miradi yote inayotekelezwa na serikali zetu mbili ile ya Muungano na hii ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakuwa na tija na kuzingatia thamani ya fedha zilizotolewa ili wakulima wapate manufaa yaliyokusudia hivyo wakandarasi wazembe hawana nafasi tena” amesema Kusaya
Awali Katibu Mkuu huyo alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo , Maliasili,Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar Mmanga Mjengo Mjawili na kumweleza kuwa uamuzi wa Viongozi wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unalenga kuwafanya wakulima wajikomboe kiuchumi kupitia Kilimo.
Aidha Kusaya amesema kupitia mradi wa ERPP serikali imelenga kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga kwa kutumia skimu za umwagiliaji ikiwa ni uhakika kwa wakulima kupata mavuno kwa kulima Zaidi ya mara mbili kwa mwaka.
Kusaya ameeleza kuwa Dkt.John Pombe Magufuli na Dkt.Ali Mohamed Shein wan Imani kuwa Kilimo cha umwagiliaji ndio njia rahisi ya kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya Kilimo nchini,hivyo usimamizi makini wa miradi hiyo yenye gharama kubwa unahitajika pande zote za nchi.
“ Nimefahamishwa kuwa uzalishaji umeongezeka baada ya skimu ya Mtwango wilaya ya Magharibi B ambapo wakulima sasa wanavuna tani 6 za mpunga toka tani 3.5 kwa hekta moja kufuatia maboresho ya miundombinu chini ya mradi wa ERPP” mesema Kusaya.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Zanzibar, Mmanga Mjengo Mjawili amesema anapongeza sana serikali zote mbili kwa usimamizi mzuri wa miradi ya kilimo ambapo wakulima wameongeza uzalishaji zao la mpunga na kufanya hali ya usalama wa chakula kuimarika visiwani .
“ Kufuatia mradi huu wa ERPP Zanzibar imeongeza uzalishaji na kuvuna mpunga toka tani 40,000 mwaka 2019 ambapo lengo ni kufikia tani 60,000 msimu wa 2020/21 hali inayochangiwa na usimamizi mzuri wa wataalam wa wizara zetu mbili” amesema Waziri huyo wa Kilimo Zanzibar
Waziri Mjawili ametoa rai kwa Makatibu Wakuu wa Kilimo Bara Gerald Kusaya na yule wa Zanzibar Maryam Abdulla kuongeza usimamizi wa karibu wa miradi hii ili wakulima na wananchi wanufaike na thamani ya fedha iliyotolewa na serikali ipatikane.
“ Tuendelee kusaidiana na kushirikiana kwa moyo ule ule wa kitanzania .Zanzibar itaweza kujitosheleza kwa chakula siku zijazo kwa kuwa sasa hali ya utoshelevu wa chakula imefikia asilimia 61” amesisitiza Mjawili
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Kusaya amekabidhi gari moja na pikipiki mbili kwa ajili ya uratibu mradi wa Kudhibiti Sumukuvu upande wa Tanzania Zanzibar
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Zanzibar Maryam Abdulla alipongeza mashirikiano kati ya Wizara yake na ile ya Tanzania Bara kupitia miradi ya TANIPAC na ERPP kuwezesha nchi zetu kuwa na uhakika na usalama wa chakula.
“ Uwepo wa miradi hii ya kilimo ni mafanikio ya Muungano wetu unavyoweza kuwanufaisha wakulima wetu.Kilimo siyo mojawapo wa mambo ya muungano lakini tunatekeleza kwa faida ya wananchi wa pande zote mbili” ameeleza Maryam
Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu ( TANIPAC) unatekelezwa kwa gharama ya Dola za kimarekani Milioni 35.3 kuanzia mwaka 2019 hadi utakapokamilika mwaka 2024 na ule wa Kuimarisha Uzalishaji Mpunga (ERPP) unagharimu Dola za Kimarekani milioni 26 tangu ulipoanza mwaka 2015 hadi utakapokamilika mwaka 2021.