Mkurugenzi wa Ufundi (WMA) Bi.Stella Kahwa kizungumza na Waandishi wa habari baada ya Semina fupi ya wafanyabiashara wadogowadogo wa sokoni iliyoandaliwa na WMA kwaajili ya kuwaelimisha kuhusu madhara ya kutumia mafungu kwenye biashara.Wafanyabiashara wadogowadogo wakifuatilia Semina fupi iliyoandaliwa na Wakala wa Vipimo kwaajili ya kuwaelimisha kuhusu madhara ya kutumia mafungu kwenye biashara. Kaimu Meneja Sehemu ya Uchunguzi(WMA),Bw.Almachius Pastory akiwaonesha wafanyabiashara wadogowadogo umuhimu wa kutumia mizani na kuachana na baishara ya mafungu.
***************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Wafanyabiashara wadogowadogo sokoni wametakiwa kutumia mizani ili kuwawezesha kupata thamani halisi kwa wanachokiuza kuliko kutumia mafungu ambapo husababisha hasara kujitokeza katika biashara zao.
Hayo ameyasema leo Mkurugenzi wa Ufundi (WMA) Bi.Stella Kahwa baada ya Semina fupi ya wafanyabiashara wadogowadogo wa sokoni iliyoandaliwa na WMA kwaajili ya kuwaelimisha kuhusu madhara ya kutumia mafungu kwenye biashara.
“Tulikuwa tunaonesha umuhimu wa kutumia mizani ambao utapelekea kwamba na wao watapata thamani halisi kwa wanachokiuza kuliko kutumia mafungu kwani utakuwa unamzidishia yule unaemuuzia”. Amesema Bi.Stella.
Aidha Bi.Stella amesema kuwa unapotumia mizani katika biashara utaweza kuuza kwa usahihi na utapata faida nzuri na utaweza kukua.
Nae Katibu wa Soko la Mburahati Bw.Fikiri Pazi ameiomba serikali itilie mkazo kwa wafanyabiashara kutumia vipimo ili kuweza kupata faida kwani kwa upande wake tokea alivyoacha kutumia vipimo amepata hasara kubwa kwenye biashara yake.
“Serikali ingetilia mkazo kwa kuweka matangazo masokoni yakabandikwa matangazo na sheria ikazingatiwa watu wengi watarudi kutumia mizani ili kuweza kupata faida”. Amesema Bw.Pazi.
Kwa upande wake Mfanyabiashara wa Soko la Ilala Bi.Veronica Mbinda ambaye anajihusisha na biashara ya njegere ameshukuru kwa semina ambayo wameipata kwani wamepata mwanga na kufahamu umuhimu wa kutumia mizani katika biashara zao.