………………………………………………………………
Na. Majid Abdulkarim, Chemba
Serikali imewataka wazazi nchini kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano za kuboresha maendeleo ya elimu kwa kuchangia upatikanaji wa chakula cha mchana shuleni ili kuwajengea wanafunzi mazingira mazuri ya kujisomea na kushindana kimasomo.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mamlaka za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Mhe. Mwita Waitara wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya juma la elimu yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Chemba iliyopo mkoani Dodoma.
Amesema bila wananchi kutia nguvu katika suala la upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi, lengo la serikali la kuhakikisha kuwa inaboresha elimu kwa kila mtoto halitafikiwa, badala yake kutaibuka matabaka kwa baadhi ya Watoto kupata chakula cha mchana na wengine kukosa kabisa.
Mhe.Waitara ameongeza kuwa wazazi hawana budi kuchangia maendeleo ya Watoto wao kwa kuhakikisha kuwa wanachangia chakula ili Watoto wote wanaosoma katika shule zote za msingi nchini wanapata chakula cha mchana shuleni.
Amesema kwa kufanya hivyo, wazazi watasaidia kupungua kwa changamoto za utoro shuleni, na kujenga mazingira mazuri ya Watoto kusoma ambapo mtoto akipata mlo wa mchana ana nafasi nzuri ya kumsikiliza mwalimu kuliko mtoto aliye na njaa.
Mhe. Waitara amesema kuwa pamoja na juhudi kubwa za Serikali ya awamu ya tano ya Mhe.Rais Dkt John Pombe Magufuli kutoa elimu bure, ikiwa baadhi ya Watoto wataendelea kusoma pasipo kupata chakula cha mchana hakutawajengea mazingira sawa ya kujifunzia.
“Hatuwezi kufanya ushindani ukawa sawa kwa kila mmoja, elimu ni bure sawa lakini kuna watoto wanashinda wakipiga miayo wakati wenzao wamekula, katika hilo unawezaje kuwa na ushindani wa kweli, lazima wengine wawe juu na wengine wabaki chini,”amesisitiza Waitara.
Mhe.Waitara ameeleza kwa kinachofanywa na serikali ni kusaidia watoto wa masikini ambao hawakuwa na uwezo wa kusoma kutokana na kukosa ada hivyo ikaamua kuwekeza huko kwa kutoa fedha jambo lililosaidia ongezeko la uandikishaji watoto wanaoanza shule.
Mapema akimkaribisha Naibu Waziri kuzungumza kwenye maadhimisho hayo, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa Bi. Annette Nara alieleza kuwa sera ya elimu bila malipo imesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza na kidato cha kwanza, na kupunguza kiasi kikubwa cha utoro wa wanafunzi shuleni.
Aidha amesema kuwa kutokana na upatikanaji wa chakula shuleni kwa baadhi ya shule zinazotekeleza kupitia Mpango wa kuboresha Elimu Tanzania (EQUIP T) ambapo wazazi wanashirikiana na walimu katika kusimamia mahudhurio ya wanafunzi.
Kabla ya Uzinduzi wa juma la Elimu Mhe. Waitara alipata fursa ya kukagua shule ya Sekondari ya Bihawana ambayo ni mojawapo kati ya shule kongwe 89 zilizopewa fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu.
Pia Naibu waziri alitembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa na kukagua ukarabati wa jengo la utawala, madarasa, mabweni, vyoo na bafu, Pamoja na miundombinu mingine ya shule hiyo iliyogharimu Shilingi 1,012,729,844.90.