Askofu Mstaafu wa Kanisa la EAGT, Evance Lucas Chande (katikati) akiwaasa watanzania kuepuka kutumiwa na baadhi wa wanasiasa wasiolitakia mema Taifa na badala yake wachangie katika kuhamasisha wananchi kuunga mkono shughuli za maendeleo yanayofanyika kwa maslahi ya wananchi. Hayo yamejiri katika mkutano uliofanyika jijini Dodoma leo Agosti 18, 2020.Shehe Abdallah Msafiri (Kushoto) ambaye ni mmoja wa viongozi wa Dini walioshiriki katika mkutano uliofanyika jijini Dodoma leo Agosti 18, 2020 ukilenga kuhimiza wananchi kulinda misingi ya amani na umoja kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2020 na kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi na kuwapuuza baadhi ya watu wanaobeza mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi hiki.
Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji wa Kipentekoste, Askofu Pius Ikongo akieleza jinsi baadhi ya wanasiasa walivyoshindwa kueleza ukweli kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na Serikali katika kipindi hiki huku wakijikita katika kupotosha ambapo aliwataka wananchi kuzingatia misingi ya amani na umoja kuelekea Uchaguzi Mkuu huku wakichagua viongozi wenye hofu ya Mungu kama alivyo Rais wa sasa Dkt. John Pombe Magufuli. Hayo yamejiri katika mkutano uliofanyika jijini Dodoma leo Agosti 18, 2020.
Sehemu ya Viongozi wa Dini walioshiriki katika mkutano uliolenga kuhimiza jamii kuzingatia misingi ya amani na umoja na kuunga mkono juhudi za kuwaletea wananchi maendeleo katika kipindi hiki.
(Picha zote na Mpiga Picha Wetu)
*************************************
Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Viongozi wa Dini wamewaasa wananchi kuepuka kutumiwa na wanasiasa wasiolitakia mema Taifa huku wakiweka mbele maslahi yao.
Akizungumza katika mkutano maalum wa viongozi wa dini Askofu Mstaafu wa Kanisa la EAGT, Evance Chande amesema kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiwatumia wananchi vibaya kwa maslahi yao hivyo kuwataka wananchi kuwaepuka na kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
“Kuelekea Uchaguzi Mkuu niwaase watanzania wote kuzingatia ulinzi wa amani iliyopo na kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kuchochewa na baadhi ya viongozi wa siasa, kama viongozi wa dini lazima tuseme ukweli na isitafsiriwe kwamba tunatumiwa na chama chochote cha siasa”, alisisitiza Askofu Chande.
Akifafanua amesema kuwa viongozi wa dini kazi yao ni kueleza ukweli ili wananchi wafanye uamuzi sahihi na wenye maslahi ya Taifa na sio watu wachache kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa ya kuleta mageuzi ya kweli kwa wananchi kupitia miradi mikubwa ya maendeleo inayoteklezwa.
Aliongeza kuwa Serikali iliyopo madarakani kwa sasa imefanikiwa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na inaendelea kuchukua hatua.
Akizungumzia umuhimu wa amani Askofu Chande amesema kuwa lazima kila mtanzania aone umuhimu wa kutunza amani kwa kuangalia mifano ya nchi jirani zilizoshindwa kutunza amani na matokea yake wahanga wakuu ni wanawake na watoto amani inapotoweka.
Kwa upande wake Shehe Abdallah Msafiri amesema watanzania hawana budi kuungana pamoja na kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ameliwezesha Taifa kuvuka salama katika janga la Corona kwa kuwa alimtanguliza Mungu na amekuwa akionesha kumtegemea Mungu katika kila jambo.
“Dini ni muhimu na ni msingi wa kujenga amani, umoja na mshikamano kwa wananchi wote hivyo viongozi wanalo jukumu kubwa la kuendelea kuhakikisha kuwa amani iliyopo inalindwa na kudumishwa kwa maslahi ya Taifa”, alisisitiza Shehe Msafiri.
Akifafanua amesema kuwa kiongozi bora ni yule anayemtanguliza Mungu kama anavyofanya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa ameiwezesha nchi kufikia maendeleo ya kweli.
Naye Katibu wa Dawati la Jinsia, Wanawake wa madhehebu ya Dini, Bi Zainabu Juma Ally amesema kuwa wanawake wanajivunia kuwa na Rais mcha Mungu na anayewajali na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuwaasa wanawake kuepuka kutumiwa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2020.
“ Tunaishukuru Serikali yetu kwa kuendelea kutekeleza miradi inayolenga kuwawezesha wananchi hasa kinamama katika maeneo yetu hasa kwa sasa ambapo wanawake wengi wamejikomboa kiuchumi”, alisisitiza Bi Zainabu.
Viongozi wa dini kutoka dini na madhehebu mbalimbali wamekutana Jijini Dodoma leo Agosti, 2020 kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2020.