Home Mchanganyiko “Taasisi za kidini sio wawekezaji kupata faida bali wanasaidiana na Serikali kufikisha...

“Taasisi za kidini sio wawekezaji kupata faida bali wanasaidiana na Serikali kufikisha huduma za kijamii” – RC Wangabo

0

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo  Mkuu wa Mkoa Wa Rukwa mh. Joachim Wangabo (katikati waliokaa) katika picha ya pamoja na watawa wa Abasia ya Roho Mtakatifu Mvimwa. (waliokaa kulia) Baba Abate Pambo Mkorwe na (waliokaa kushoto) Frt. Gualbert Mgaya aliyekuwepo tangu kuanzishwa kwa Abasia hiyo. 

************************************

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi wanaoishi karibu na maeneo yanayomilikiwa na taasisi za kidini kuacha kuzitazama taasisi hizo kama kampuni za uwekezaji na badala yake washirikiane nazo katika kuleta maendeleo ya eneo husika ili amani iendelee kutawala katika Mkoa nan chi kwa ujumla.

Amesema kuwa Taasisi hizo zimekuwa zikijenga mashule na hospitali kwaajili ya kusogeza karibu huduma hizo kwa jamii na kwa kufanya hivyo wanasaidiana na serikali katika kuhakikisha wananchi hawasumbuki kwenda umbali mrefu kupata huduma hizo na kuongeza kuwa mbali na huduma hizo za kijamii pia taasisi hizo hutoa huduma za kiroho ambazo zimetawaliwa na ujumbe wa amani na upendo.

Akizungumza baada ya kushiriki ibada ya Jumapili (16.8.2020) katika Kanisa la Abasia ya Roho Mtakatifu Mvimwa kata ya Kate wilayani Nkasi, Mh. Wangabo aliridhwa na hatua zilizochukuliwa na serikali katika kutatua tatizo la mgogoro uliokuwepo baina ya wananchi na Abasia hiyo jambo lililopelekea wananchi kuelewa na kukubali kazi za Abasia hiyo.

“Ni pongezi kubwa sana, hapa mahali kulikuwa na mgogoro kipindi Fulani huko nyuma baina ya hii Congregation (Jumuia) ya hapa Mvimwa na Kijiji cha Ntemba, (wananchi) walikuwa hawaelewi kabisa mpaka mmejenga ile shule ya msingi pale, madarasa zaidi ya saba kama sikosei na maji mmechima, sasa hivi kuna utulivu, mafuriko ya Wanafunzi, sasa wamewaelewa kumbe mnaishi kwaajili ya jamii, Wananchi niwaombe muielewe hii jumuia, iko kwaajili ya wananchi haiko hapa kunyanyasa wananchi hapana hawa sio wawekezaji wa kutafuta faida, muwape ushirikiano” Alisema.

Aidha, Mh. Wangabo amesifu kazi zinazofanya na Abasia hiyo katika kuimarisha fani mbalimbali kwa wananfunzi wanaosoma shule ya ufundi pamoja na shule ya msingi na sekondari na kuwashauri vijana kuachana na fikra za zamani za kungoja kuajiriwa badala yake waelekeze visomo vyao katika kujitegemea.

“Wengine wanadhani bado tunaishi zama zile kwamba unasoma ili uajiriwe, unasoma sasa hivi ili ujitegemee, ndio dhana tuliyonayo, zamani tulisoma wachache na watumishi walikuwa wachache, kwahiyo akili zote zilikuwa kwenye kupata ajira, lakini sasa hivi wasomi ni wengi sana na nafasi za kiutumishi wa seikali ni chache, kwahiyo someni ili mjitegemee, muendeshe Maisha yenu kupitia kile ulichojifunza na ukifanye kwa umahiri mkubwa,” Alisisitiza.

Kwa upande wake Baba Abate Pambo Mkorwe wa Abasia ya Roho Mtakatifu Mvimwa amesema kuwa wanafunzi wanaopita katika mikono ya shule zilizopo chini ya Abasia hiyo wanajengewa misingi ya kuendeleza gurudumu la maendeleo na kuongeza kuwa mchocheo wa Abasia hiyo ni Sala na Kazi na hivyo kazi kubwa kuandaa wasomi wenye kupenda kufanya kazi na sio kinyume chake.

“Tunataka tuunde wasomi ambao wana ari ya kufanya kazi, kuna bahati mbaya ya kuwa na wasomi ambao ni wavivu, wasiopenda kufanya kazi. Wanaopita mikononi mwetu tunapenda washiriki pia katika roho yetu ya kazi ili kuyaemeza maisha yao, katika mtazamo huo hata ukienda shule ya msingi utakuwa kuna mifugo na bustani pia, ambao Watoto wenyewe wanashiriki katika shughuli hizo na wakitoka hapo wanakuwa wamekomaa,” Alisema.

Pia Baba Abate Mkorwe alitoa shukrani zake kwa mkuu wa mkoa kwa kuhakikisha Abasia hiyo inafikiwa na umeme tangu kuanzishwa kwake mwaka 1979 huku tayari wakiwa wametimiza miaka 41 bila ya kuwa na umeme wa serikali.

Katika hatua nyingine Mh. Wanagabo amewataka waamini waliohudhuria katika ibada hiyo kuwa watulivu wakati nchi ikiwa imebakiza siku chache kuingia kwenye kampeni za uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Rais na hivyo kuwashauri wachague viongozi bora watakaoweza kutatua kero zao