Home Mchanganyiko NAIBU WAZIRI WA NISHATI AWATAKA WAKANDARASI KUFANYA KAZI KWA WELEDI

NAIBU WAZIRI WA NISHATI AWATAKA WAKANDARASI KUFANYA KAZI KWA WELEDI

0

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika katika kijiji cha Ilula, kata ya Ilula, Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiongea na wananchi (hawapo pichani)wa  katika kijiji cha Ilula, kata ya Ilula, Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza,kabla ya kuwasha umeme kwenye kijiji hicho

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(wa pili kulia) akikata utepe kuashiria kuwashwa kwa umeme katika shule ya Sekondari Imalilo, Iliyopo kwenye kijiji cha Kibitilwa, Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza

Wananchi wa kijiji cha Busolwa ,kata Igokelo, Wilaya ya Misungwi , Mkoani Mwanza, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(hayupo pichani) wakati akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa kazi za usambazaji umeme vijijini

 

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(mwenye shungi) akiwa katika picha ya Pamoja na wafanyakazi wa kampuni ya ETDCO,katika kijiji cha  Busolwa ,kata Igokelo, Wilaya ya Misungwi , Mkoani Mwanza, wakati akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa kazi za usambazaji umeme vijijini

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwa Pamoja na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Imalilo,iliyopo kwenye kijiji cha Kibitilwa,kata ya Ilula, Wilaya ya Kwimba, wakati akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa kazi za usambazaji umeme vijijini

…………………………………………………………………………..

Hafsa Omar-Mwanza

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi  wanaofanya kazi za usambazaji umeme vijijini kufanya kazi zkwa weledi, uaminifu na kwa kasi ili kuweza kufanikisha kazi zao kwa wakati.

Ameyasema hayo, Agosti 15,2020 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Busolwa, kata ya Igokelo Wilaya ya Misungwi,Mkoani Mwanza, wakati akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme vijijini.

Aidha, amesema Serikali haitasita kusitisha mkataba wa mkandarasi yoyote nchini ambae hataendana na kasi ya Serikali ya awamu ya Tano.

“ Nataka nitoe wito kwa wakandarasi kufanya kazi kwa bidii kwasababu Wananchi wanahitaji huduma ya umeme,na bila ya jitihada kubwa za wakandarasi za kufanya kazi kwa bidii hii itasababisha wakandarasi hao  kushindwa kumalizia kufanya kazi katika maeneo yao”alisema.

Vilevile ,amesema Serikali imeamua kutoa nafasi kwa wakandarasi wazawa kufanya kazi ya usambazaji umeme ili kuwawezesha wananchi wake waweze kujiajiri na kujiimarisha katika kazi zao.

“Tangu tumeingia kwenye Wizara zaidi ya mara kumi tumekuwa tukifanya vikao mbalimbali na wakandarasi mjini Dodoma tukifanya tathmini na kutolea maagizo mbalimbali ili kuona namna bora ya kuweza kuwasaidia wakandarasi hao kuweza kufanya kazi kwa weledi”alisema Mgalu

Pia amesema, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lina wataalamu wa kutosha na wenye uwezo wa kufanya kazi ambazo zinafanywa na wakandarasi wengine, lakini Serikali iliamua kutoa nafasi kwa wakandarasi binafsi nafasi ambayo baadhi ya wakandarasi wamshindwa kuitumia vizuri.

Vilevile, ameipongeza  kampuni ya ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya Tanesco ambayo kwasasa ndio inayohusika na kazi ya usambazaji  umeme vijijini Mkoani Mwanza.

“ Nimekuja kukagua kazi inayofanywa na mkandarasi ambae amechukua nafasi ya mkandarasi Nipo group lakini tangu nimeanza kukagua nimeona ETDCO inafanya kazi nzuri sana,”alisema.

Naibu Waziri, pia amemtaka mkandarasi huyo kufanya kazi hiyo kwa haraka zaidi kwakuwa wananchi wa vijiji hivyo wanasubiri huduma ya umeme kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda ameiomba Serikali iendelee kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Misungwi hasa katika maeneo ya migodi maeneo ambayo wananchi wengi wamejiajiri kwenye maeneo hayo.

Katika ziara yake hiyo, Naibu Waziri aliwasha umeme katika zahanati ya kijiji Ilula na katika Shule ya Imalilo iliyopo katika kata ya Ilula Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza.