Home Mchanganyiko MSAKO WA NYUMBA KWA NYUMBA KWA WAUZA NA WATUMIAJI POMBE HARAMU WAANZA...

MSAKO WA NYUMBA KWA NYUMBA KWA WAUZA NA WATUMIAJI POMBE HARAMU WAANZA RASMI

0

Kijana Abrahman Ismail akiwa amebeba mizigo yake kuashiria kuhama katika banda alilokuwa anaishi baada ya wananchi wa Kijiji cha Minazini shehia ya Tibirinzi wilaya ya Chake Chake Pemba kumata ahame kutokana na tabia yake ya ulevi (Picha na Masanja Mabula)

…………………………………………….

Na Masanja Mabula , Pemba.

Wakazi wa kijiji cha Minazini Shehia ya Tibirinzi wilaya ya Chake Chake wameanzisha msako wa nyumba hadi nyumba kuwasaka wauzaji  na watumiaji wa pombe haramu aina ya gongo pamoja na madawa ya kulevya.

Msako huo uliosimamiwa na polisi Jamii wa kijiji hicho ulifanikiwa kuwakamata vijana wawili wanaodaiwa kuwa ni watumiaji wa pombe haramu aina ya gongo na madawa ya kulevya.

Mmoja wa kijana aliyekamatwa akituhumiwa kuwa mtumiaji maarufu wa pombe haramu aina ya gongo ,Abdulrazak Ismail akilazika kuhama katika kijiji hicho baada ya jamii kukosa imani naye wakidai amekuwa ni chanzo cha uvunjifu wa maadili.

Akizungumza baada ya msako huo Mwenuyekiti wa Polisi jamii aliwataja vijana waliokamatwa kuwa ni Abdulrazak Ismail pamoja na Said Mohammed.

Aidha alisema mbali ya kuwasaka watengenezaji na watumiaji wa pombe haramu aina ya gongo, pia utasaidia kukudhibiti wahalifu kutoka maeneo mengine ambao wamekuwa wakikimbia katika kijiji hicho baada ya kufanya uhalifu katika maeneo yao.

“Kwa kipindi sasa kijiji chetu kimekuwa ni maficho ya wahalifu , ambao wamekuwa wakikimbilia na kujificha baada ya kufanya uhalifu katika maeneo yao”alifahamisha.

Naibu wa sheha wa shehia ya Tibirinzi Hamid Said Mohammed alisema pamoja na mafanikio ya kupunguza wimbi la utengenezaji na utumiaji wa pombe haramu aina ya gongo, lakini bado wapo baadhi ya wananchi wanaendelea na biashara hiyo.

“Kwa kweli tumefanikiwa kwa asilimia 80, lakini bado asilimia 20 ambazo zinahitaji nguvu ya pamoja kutoka serikali kuu na jeshi la Polisi ili kutokomeza matendo hayo”alisema.

Kwa upande wake Kijana Abrahman Ismail akizungumza wakati akiwa anakunja mizigo yake alisema bado Polisi jamii hawaja tayari kudhibiti hali hiyo kwani yeye ni mtumiaji tu.

“Wanaotengeneza wanafahamika, na mimi naenda kunywa huko huko na sifanyi vitendo vya uvunjifu wa maadili, hivyo hawa Polisi jamii wanapaswa kuwashughulikia kwanza wanaotengeneza na sio watumiaji”alisisitiza.

Aidha alifahamisha kwamba , kwa siku anatumia shilingi elfu tatu kununua pombe hilo na kuahidi kuachana na matumizi ili kurejesha afya yake.