Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Omary Mgumba (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe.Loata Olesanare (kushoto) mara baada ya mazungumzo yao ofisini kwa mkuu huyo wa mkoa leo
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Olesanare (kushoto) akiagana na Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (TANIPAC) Clepin Josephat leo mara baada ya kikao ofisi kwake.Katikati ni Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Omary Mgumba. Mradi wa TANIPAC utajenga ghala la kisasa katika kijiji cha Chakware wilaya ya Gairo kwa ajili ya kuhifadhia nafaka tani 2,000 kwa gharama za shilingi Bilioni moja mwaka huu.
Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akiongea na wananchi wa kitongoji cha Ukwamani wilaya ya Gairo leo kuhusu kuacha tabia ya kuanika mahindi chini hali inayoweza sababisha yaathiriwe na fangasi wanaosababisha sumukuvu.
Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba ( wa kwanza kulia) akikagua eneo kutakapojengwa ghala la kisasa chini ya mradi wa Kudhibiti Sumukuvu katika kijiji cha Chakwera wilaya ya Gairo alipofanya ziara ya kikazi leo.
…………………………………………………………………………..
Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba amewashauri wakulima wa mazao
ya mahindi nchini kuacha kuanika mazao yao chini ya ardhi ili kuepuka
yasichafuliwe na fangasi wanaosababisha sumukuvu.
Ametoa agizo leo katika kijiji cha Chakware wilaya ya Gairo
wakati alipotembelea kuhamasisha wakulima na wafanyabiashara
kuzingatia kanuni bora za uhifadhi wa mazao ili kudhibiti tatizo la
sumukuvu linaloaathiri mazao hayo.
“ Nipo hapa Gairo kuwahamasisha wakulima wote hususani wale wa zao la
mahindi kuacha tabia ya kuanika mahindi kwenye ardhi kwani inapelekea
yachafuliwe na fangasi wanaosababisha sumukuvu ambayo ni hatari kwa
afya ya wanadamu” alisema Mgumba
Aliongeza kusema Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani
imejidhatiti kuhakikisha tatizo la sumukuvu kwenye zao la mahindi na
karanga linadhibitiwa kwa wakulima na wafanyabiashara kupatiwa elimu.
Naibu Waziri Mgumba amesema Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (Tanzania
Initiative To Prevent Aflatoxin Contamination-TANIPAC) unatekelezwa
kwenye mikoa kumi ya Tanzania Bara na miwili ya Zanzibar kwa gharama
ya Dola za kimarekani Milioni 35.1 ( sawa na shilingi Bilioni 80) tangu
mwaka 2019 .
“ Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kuhakikisha
wananchi wanafundishwa elimu ya kuepukana na sumukuvu ili isiendelee
kuathiri maisha ya watu na kupoteza mazao ya wakulima” alisema Naibu
Waziri Mgumba
Ametaja faida za mradi huo wa TANIPAC kwa nchi kuwa utasaidia kuokoa
upotevu wa mazao baada ya mavuno kwa kuongeza uhifadhi bora wa
mazao na pili utasaidia kuongeza kipato cha mkulima na mfanyabiashara
kwa kuzuia sumukuvu kuathiri mazao
Tatu mradi huo umelenga kuokoa nguvukazi ya watanzania kwa
kuhakikisha chakula kinacholiwa kinakuwa hakichafuliwa na fangasi aina ya
kuvu .
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe ameiomba
wizara ya Kilimo kusaidia kuimarisha ushirika ili wakulima wa zao la
mahindi na mazao ya mbogamboga ambayo yanastawi vema wilayani
humo kupata soko la uhakika.
Mchembe amesema wilaya ya Gairo ndio inaongozwa kwa uzalishaji wa
mahindi kwenye mkoa wa Morogoro ambapo msimu huu 2019/2020
imevuna tani takbribani 40,000 na kuwa uwepo wa mradi wa TANIPAC
utaongeza uwezo wa kuhifadhi na wakulima kunufaika.
Akizungumzia kuhusu mradi wa ujenzi wa ghala la kisasa la kuhifadhi
mahindi ,Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (TANIPAC) Clepin
Josephat amesema ghala litakalojegwa kijijicha Chakware litakuwa na
uwezo wa kuhifadhi tani 2,000 za nafaka litakapokamilika.
“ Mradi wa TANIPAC utajenga ghala la kuhifadhia nafaka lenye uwezo wa
tani 2,000 kwa gharama za shilingi Bilioni Moja ili kusaidia wakulima
kupata mahala pa kuhidadhi mazao yao na kupata elimu ya udhibiti wa
sumukuvu katika kipindi cha miaka mitano ya mradi huu” alisema Clepin.
Clepin aliongeza kusema mradi wa TANIPAC umelenga kuhakikisha elimu
kwa wakulima juu ya madhara ya sumukuvu inawafikia vijijini na pia
kujenga miundombinu bora ya kuhifadhi mazao ili yasichafuliwe na
sumukuvu hivyo kuongeza faida kwa biashara ya mazao.