Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Mwalusembe wilayani Mkuranga wakati alipofanya ziara ya kushitukiza Shuleni hapo, Agosti 13, 2020.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
…………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wiki mbili kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa wilaya ya Mkuranga na Mkurugenzi Mtendaji wake wahakikishe shule za msingi na sekondari za Mwarusembe zinakuwa na madawati.
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Agosti 13, 2020) wakati akizungumza na wananfunzi na walimu wa shule ya msingi Mwarusembe alipofanya ziara ya kushtukiza katika shule hiyo na kukuta baadhi ya wanafunzi wamekaa chini.
“Nawapa wiki mbili nikija nikute madawati hapa na kule kwenye shule ya sekondari Mwarusembe. Nimeambiwa wananfunzi wa kidato cha kwanza pale sekondari, hawana madawati. DC upo, Mkurugenzi upo, na unajua hali yako ilivyo, unafanya nini?”
“DC, Mkurugenzi na Mkuu wa Mkoa kama hali ni hivi hapa Mwarusembe ambapo ni jirani na barabara kuu, je hali ikoje huko ndani vijijini?,” alihoji Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alisema mkoa huo unaongoza kwa idadi kubwa ya viwanda, na wilaya hiyo peke yake ina viwanda 75 lakini haijaweza mbinu za kupata madawati. “Halmashauri yenu ina viwanda vingi kuliko wilaya zote, hivi vyote vinafanya nini? Kwa nini msiende kwenye viwanda vyenu mkaongee nao ili fedha ya CSR itumike kuondoa tatizo hili? Mapato yenu kwa mwaka ni zaidi ya shilingi bilioni mbili, zinafanya nini?”
“Viwanda vipo vingi, vingine vya mbao, vingine vya vyuma na vya saruji halafu mnasema hakuna madarasa ya kutosha. Kwa nini msiunganishe nguvu na kuondoa hili tatizo? Kwa nini mnasubiri Mheshimiwa Rais aje apewe malalamiko na wananchi?,” alimhoji Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Bw. Filbert Sanga.
Waziri Mkuu amesema ukosefu wa madawati unawafanya walimu washindwe kusimamia usafi kwa wanafunzi lakini pia unawapa mzigo wazazi wa kununua sabuni ili watoto wao wafue nguo kila siku.
“Nataka Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri na wakuu wa idara hasa wa elimu mjipange upya katika suala la madawati. Nikija tena na nisipokuta madawati, mjiandae…”