Mkufunzi Mwandamizi Kilimo cha Bustani ya Mbogamboga wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Mati Mtwara, Ashraf Mohammed (kulia) akizungumza na wananchi waliotembelea shamba la mbogamboga la mfano la chuo hicho wakati wa Maonesho ya NaneNane 2020 yaliyofikia tamati hivi karibuni katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Mkuu wa chuo hicho, Elias Maijo, akizungumzia historia ya chuo na shughuli wanazozifanya.
Mwanafunzi Masudi Masudi (kulia) akizungumzia kilimo hifadhi.
Mratibu wa Masomo wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Mati Mtwara, Doroth Moshi (kulia) akizungumza na wanafunzi wa Sekondari ya Chungutwa walipotembelea banda la chuo hicho wakati wa Maonesho ya NaneNane 2020 yaliyofikia tamati hivi karibuni katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Mratibu wa Masomo ya muda mfupi wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Mati Mtwara, Muhaji Lenga (kulia), akizungumza na wananchi waliotembelea banda la chuo hicho wakati wa Maonesho ya NaneNane 2020 yaliyofikia tamati hivi karibuni katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Mkufunzi Kilimo wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Mati Mtwara, Amoni Mtono (kushoto) akizungumza na wanafunzi wa Sekondari ya Chungutwa walipotembelea shamba la mfano la chuo hicho wakati wa Maonesho ya NaneNane 2020 yaliyofikia tamati hivi karibuni katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Mkufunzi Kilimo wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Mati Mtwara, Mawazo Gadafi (kulia) akizungumza na wananchi waliotembelea shamba la mfano la matango chuo hicho wakati wa Maonesho ya NaneNane 2020 yaliyofikia tamati hivi karibuni katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Mkufunzi Kilimo wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Mati Mtwara, Idara ya Vipando, Daud Kasabuka (kushoto) akizungumza na wananchi waliotembelea shamba la mfano la chuo hicho wakati wa Maonesho ya NaneNane 2020 yaliyofikia tamati hivi karibuni katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Mwonekano wa shamba la mfano la chuo hicho wakati wa Maonesho ya NaneNane 2020 .
Mwonekano wa Kitalu Nyumba katika chuo hicho.
Mkufunzi na Msimamizi Mkuu wa Mashamba ya Chuo cha Kilimo Mati Mtwara, Luca Chiwalo, akizungumzia kilimo cha zao la korosho kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) waliotembelea shamba la chuo hicho hivi karibuni lililopo Naliendele mkoani humo.
Mwanafunzi Werusi Nyirenda wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Mati Mtwara, (kushoto) akizungumza na mkulima Christina Mwita alipotembelea shamba la mfano la matango la chuo hicho wakati wa Maonesho ya NaneNane 2020 yaliyofikia tamati hivi karibuni katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
.
Mwonekano wa shamba la matango la mfano la chuo hicho wakati wa Maonesho ya NaneNane 2020
Mwonekano wa bustani ya mfano ya chuo hicho wakati wa Maonesho ya NaneNane 2020
Mwanafunzi Adam Mwangonela akizungumzia kilimo cha mbogamboga.
Mwanafunzi Franco Kabakama akizungumzia kilimo cha matango.
Mwanafunzi Geofrey Mkinga akizungumzia kilimo hifadhi.
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo cha Kilimo Mati Mtwara, Elizabeth Msambaa, akionesha jinsi ugonjwa wa ubwiliunga unavyoathiri maua ya mikorosho wakati waandishi wa habari walipotembelea shamba la chuo hicho hivi karibuni lililopo Naliendele mkoani humo.
Mwanafunzi Ester Mtajia akizungumzia kilimo cha korosho.
Mwanafunzi Legneth Magubika akizungumzia kilimo cha korosho na faida zake.
Mwanafunzi Yahaya Mtego akizungumzia kilimo cha korosho na jinsi ya utunzaji wa mashamba
Shughuli ya upuliziaji dawa ya kuuwa wadudu kwenye mikorosho ikifanyika.
Na Dotto Mwaibale, Mtwara
CHUO cha Mafunzo ya Kilimo cha ‘Mati Mtwara’ kimezidi kung’ara na kusonga mbele kwa kupanua wigo kwenye eneo la mafunzo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo, na sasa kipo mbioni kuboresha mfumo wake wauzalishaji mali ili kwenda sambamba na mahitaji ya soko.
Mkuu wa chuo hicho, Elias Maijo , alibainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea chuo hicho kilichopo Naliendele, mkoani Mtwara wakati wa Maonesho ya NaneNane 2020 yaliyofikia tamati hivi karibuni katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
“Shabaha yetu kwa sasa ni kuboresha‘model’ ya uzalishaji ili kwenda sanjari na mahitaji ya soko. Msisitizo wetu mkubwa ukiwa ni kuanza kuzalisha kwa kuzingatia tafiti zetu kuhusu mahitaji ya soko,” alisema Maijo.
Alisema chuo hicho chenye uwezo wa kupokea zaidi ya wanafunzi 362 bado kina fursa nyingi kwa tija na mabadiliko chanya kwenye eneo la uchumi wa viwanda, huku akiomba serikali na wadau kutoa msukumo wa kipekee, hususan kwenye rasilimali fedha kukiwezesha kukarabati miundo mbinu na vifaa chakavu sanjari na kuanzisha miradi mipya.
Maijo alisema kwa sasa wamejikita katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, biashara kama korosho, bustani na ufugaji bora wa mifugo kama ng’ombe, mbuzi, kuku na nguruwe ambao hutumika kuwafundishia wanafunzi na wakulima.
“Tunafundisha wanafunzi ambao ni maafisa ugani tarajiwa na mfumo wa hapa Mati Mtwara tunatumia zaidi vitendo kuliko nadharia, lengo letu hasa ni kuwawezesha wahitimu kutoka na teknolojia stahiki kama wataalamu kwa tija na ustawi wa taifa,” alisema.
Mkuu huyo alisema chuo hicho kilianzishwa mwaka 1974 na kuanza utoaji wa masomo rasmi Juni 19, 1975 kwa kozi ya Stashahada ya kilimo mseto kwa wakati huo kwa ufadhili wa mradi wa International Development Agency (IDA) lengo lake kubwa likiwa ni kutoa mafunzo zaidi kwa wanafunzi na wakulima ili kupata wafanyakazi wenye ujasiri na uwezo kwa ajili ya kujiajiri na kuajiriwa serikali au katika mashirika mbalimbali.
“Lengo lingine lilikuwa ni kuchukua teknolojia zinazozalishwa na watafiti chuoni hapa na kuzisambaza kwa wakulima ili kuongeza tija na kuwa na usalama wa chakula hapa nchini” alisema Maijo.
Alisema hayo ni malengo mahususi ya kuanzishwa kwa chuo hicho ambacho ni miongoni mwa vyuo 14 vilivyopo hapa nchini ambavyo vipo chini ya Wizara ya Kilimo.
Alisema kutoka kipindi hicho chuo kimekuwa kikichukua wanafunzi katika ngazi ya Astashahada pamoja na diploma na tangu wakati huo takriban wahitimu 4000 wamehitimu.
Aidha, Maijo mbali ya kuipongeza serikali kwa jitihada kadhaa za uboreshaji wa vyuo vyake, aliomba changamoto kadhaa zilizopo chuoni hapo kupewa msukumo wa kipekee, ikiwemo tatizo la uhaba na uchakavu wa vitendea kazi na miundombinu muhimu ili kuleta tija na kuongeza kasi ya uwajibikaji.
“Tunampongeza Rais Magufuli kwa kutilia mkazo uboreshaji wa kilimo kwa lengo la kupata malighafi za viwanda ambavyo kwa sasa ndio injini ya kutufikisha kwenye uchumi wa kati na kujitosheleza kwa chakula,” alisema Maijo.
Maijo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wakulima na wadau mbalimbali kufika katika chuo hicho kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo kutoka kwa wakufunzi wabobezi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Masomo wa chuo hicho kilichopo kilomita 12 kutoka Mtwara mjini chenye ukubwa wa ekta 560, Doroth Moshi alisema wanatoa kozi za aina mbili za muda mrefu na muda mfupi na kuwa kwa kozi ya muda mrefu wanatoa kozi ya Stashahada na Astashahada za kilimo.
Alisema katika Stashahada ya kilimo wanatoa diploma ya miaka miwili na mwaka mmoja ambapo diploma ya miaka miwili inawahusisha waombaji waliomaliza kidato cha sita na kufaulu walau alama moja moja katika masomo ya sayansi.
Aliongeza kuwa kwa Astashahada ya kilimo hiyo ni kozi inayochukua miaka miwili na kuwahusisha waombaji waliomaliza kidato cha nne na kufaulu walau masomo manne kwa kiwango cha D na katika D nne mbili ziwe za masomo ya sayansi.