…………………………………………………………………………….
NA.Alex Sonna,Dodoma.
SERIKALI imeagiza kuchunguzwa kwa kuthibitishwa kwa mbegu za uhandisi jeni (GMO) zinazodaiwa kuwa na viashiria vya kuendeleza njaa barani Afrika kama kweli zinafaa kwa matumizi na zitaweza kusalia nchini na bara la Afrika kwa kipindi kirefu.
Agizo hilo limetolewa leo jijini hapa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mussa Zungu wakati akizundua Kamati ya Kitaifa ya Matumizi Salama ya Bioteknolojia ya Kisasa.
Kamati hiyo ina kazi ya kuishauri Serikali ikiwa ni pamoja na kupitia maombi ya matumizi ya viumbe na bidhaa zitokanazo na biotejinolojia ya kisasa na kushauri kuhusu Sera, Sheria, tafiti na ushiriki wa sekta binafsi na umma kwa ujumla katika matumizi ya biotekinolojia ya kisasa.
Mheshimiwa Zungu amesema kuna habari zinatembea ambazo hazijathibitika na inawezekana vilevile kuna baadhi ya Product ‘bidhaa’ mpya ambazo zinaletwa nchini au afrika zina mkakati mrefu wa kuendeleza njaa barani Afrika.
Ameieleza kamati hiyo kuwa hiyo ni kazi yao kuchunguza na kuthibitisha GMO hizo kama kweli zinafaa ndani na zitaweza kusalia nchini na bara la Afrika kwa kipindi kirefu.
Ameweka wazi kuwa vita kubwa duniani inakuja sera ikiwa ni chakula na maji vikikosekana taifa litaangamia lakini anaamini kuwa majukumu na uzalendo waliopewa kamati hiyo watasimamia vizuri tafiti na kushauri serikali njia ipo sahihi ambayo nchi itatumia.
Amefafanua kwa kawaida tafiti hizo zilishafanywa muda mrefu lakini hazifanyiwi kazi zinakaa chini ya meza, pembeni na taifa linaangamia licha ya tafiti kufanyika.
“Nakumbuka miaka ya nyuma mpango wa maendeleo wa Tanzania haukutumika vizuri lakini ulitumika vizuri nje za nje miaka 80 na miaka 90 mpango wa maendeleo wa nchi yetu yalichukuliwa na nchi nyingine sisi wenyewe tuliyaweka chini ya meza
Lakini kwa awamu hii ya tano mabadiliko mmeyaona ya Rais Dkt. John Magufuli kwa uazalendo wake na upenzi wake wa Taifa letu linaendelea na litazidi kuwa hivyo kwa tafiti na maoni na mapendekezo ambayo mtaipa serikali ili tuweze kuvuka,”amesisitiza.
Aidha, Mheshimiwa Zungu ameiagiza kamati hiyo kuhakikisha inasimamia vizuri tafiti inazofanya kuhusu bioteknolojia ya kisasa na kuishauri serikali ili ijue ni njia ipi sahihi ambayo nchi inapaswa kutumia ili kuhakikisha kunakuwa na usalama na faida ya matumizi yake
Amebainisha kuwa kwa kuzingatia umuhimu wa biotekinolojia ya kisasa na madhara yanayoweza kujitokeza, Serikali imeandaa na kuweka nyenzo mbalimbali za usimamizi wa teknolojia hiyo.
Ametaja nyenzo hizo kuwa ni pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Matumizi Salama ya Bioteknolojia ya Kisasa (National Biosafety Framework), 2007.
Aidha, Kanuni za Matumizi Salama ya Bioteknolojia ya Kisasa ya mwaka 2009 (Biosafety Regulation) na marekebisho yake ya mwaka 2015, Miongozo mbalimbali (Biosafety Guidelines and Mannuals) za mwaka 2010.
Ameeleza kuwa hadi sasa mfumo wa usimamizi umewezesha kufanyika kwa utafiti ndani ya maabara wa mihogo unaolenga kupata ukinzani dhidi ya magonjwa ya virusi vya zao la Muhogo, utafiti nje ya maabara wa mahindi yanayovumilia ukame na Bungua, kusafirisha chakula cha msaada kupitia bandari ya Dar es salaam kwenda nchi jirani.
Hata hivyo, amesema pamoja na hatua hizo bado kuna changamoto mbalimbali zinazokabili eneo hili ikiwa ni pamoja na uelewa mdogo miongoni mwa jamii kuhusu biotekinolojia ya kisasa, uchache wa wataalam wa masuala ya biotekinolojia ya kisasa na usimamizi wake.
Vilevile, uhaba wa miundombinu hususan vifaa utambuzi na ung’amuzi wa bidhaa au mazao yatokanayo na biotekinolojia ya kisasa na kueleza kuwa ni mategemeo yake kuwa, Kamati hiyo itajielekeleza katika kushauri namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo.
Amesisitiza kuwa, katika kutekeleza majukumu yao, itakuwa vyema baada ya kikao chao cha kwanza wakaandaa mpango kazi wa utekelezaji wa mjaukumu yao kwa kipindi cha miaka mitatu utakaoonesha namna kamati hii itakavyosaidia kuboresha jukumu la kihakikisha kuwa Tanzania inafaidika na matumizi ya tekinolojia hiii kwa maendeleo endelevu.