Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kitumba (hawapo pichani) kabla ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Mipango unaofanyika kwenye kijiji hicho jana. Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Mipango , Profesa Martha Qorro, akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho tawi la Mwanza unaofanyika katika Kijiji cha Kitumba, wilayani Magu. Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Mipango , Profesa Martha Qorro (kushoto), akimuongoza Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho tawi la Mwanza unaofanyika katika Kijiji cha Kitumba, wilayani Magu.
******************************
MRADI wa ujenzi wa Chuo cha Mipango (IRDP) Tawi la Mwanza unaotekelezwa kwa gharama ya sh. bilioni 2.4 unatarajiwa kukamilika Januari 2021 tayari kupokea wanafunzi na kutumika kwa masomo.
Hayo yalielezwa na Mhandisi Hashimu Mzava, wakati akitoa taarifa fupi kwa Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli , alipotembelea na kukagua mradi huo unaotekelezwa katika Kijiji cha Kitumba katika Kata ya Kisesa jana.
Mhandisi Mzava, anayesimamia ujenzi huo kutoka Chuo Kikuu cha Mbeya alisema majengo mawili ya mradi huo yamegharimu sh. bilioni 2.4 na yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,200 kwa wakati mmoja.
“Ujenzi ulianza Machi 10, 2020 na utakamilika Januari 9, 2021.Watendaji na ajira zote zimepatikana Magu na tayari majengo mawili ya kumbi za mikutano kila moja likiwa na kumbi mbili ambapo mkubwa utabeba watu 400 na mdogo 200 yamebaki kuezekwa ili wanafunzi waanze masomo mwakani,”alisema.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Profesa Martha Qorro, alisema chuo hicho kinashughulika na mipango ya maendeleo vijijini na kutoa fursa kwa jamii na wananchi kushiriki wanayojifunza ili pia wayapate .
“Nawashukuru wananchi wa Kijiji cha Kitumba kwa kutupokea na kutupatia ardhi ya kujenga chuo hapa ili Watanzania wanufaike na utaalamu na mipango ya maendeleo kupitia kwa wataalamu wanaoandaliwa na Chuo cha Mipango,”alisema.
Profesa Qorro alisema uongozi na watumishi wa chuo hicho wanafarijika kuona mipango iliyokwama awamu zilizopita ikikwamuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli na hivyo wananchi hawana budi kuiunga mkono kwa namna ilivyoboresha sekta ya elimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo alisema uwekezaji uliofanywa na Chuo cha Mipango kujenga chuo Magu ni wa busara kwa sababu watasoma watoto wa Watanzania na kupata elimu itakayowasaidia kuendesha mipango ya maendeleo na maisha yao.
Alisema kwa vile serikali inasimamia maendeleo ya wananchi ni vyema vyuo vingine vyenye nia ya kuwekeza wilayani humo vikaiga mfano wa Chuo cha Mipango kwani serikali imeweka mazingira mazuri ambapo Magu ni eneo salama, ni pazuri nia watu wapate elimu ya kusaidia.
Alieleza kuwa Rais Dk. John Magufuli amefanya mengi makubwa yaliyowafanya wananchi kuondoka kwenye ujima na kuiingia kwenye uchumi wa kati na hivyo Watanzania wakiwemo wananchi wa Magu hawana budi kuyaenzi yaliyofanywa na Rais.
“Wananchi wa Magu hawana cha kuwalipa zaidi ya kuwa walinzi wa miundombinu ya chuo inayojengwa kwa gharama kubwa.Chuo cha Mipango hiki ni cha pili Barani Afrika, baada ya Misri hivyo wananchi wasisite kupata na kutumia kompyuta kufany mipango yao kwa sababu umeme upo hadi vijijini,”alisema Kalli .
Awali Mkuu wa Chuo cha Mipango, Profesa Hozen Mayaya alisema ili kuhimili uchumi wa kati mipango madhubuti inahitajika na ni lazima maendeleo yapangwe kwa kuwatumia wataalamu wa mipango kwa kuwa uchumi huo unaambatana pia na vitendea kazi vya teknolojia ya kisasa.
Alisema uongozi wa chuo unawashukuru wananchi wa Kitumba wilayani Magu kwa kukubali kutoa eneo la kujenga chuo hicho ili kulisukuma taifa kwenye sekta ya elimu.
“Kupanga ni Kuchagua, mwaka huu wa fedha tutajenga jengo la utawala, makazi ya wanafunzi , kantini na jengo jingine kubwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,”alisema mkuu huyo wa chuo