Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akitangaza bei mpya ya Mbolea kwa msimu wa mwaka 2020/2021 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi mdogo wa Wizara ya Kilimo Maarufu kama “Kilimo IV” ofisini kwake Jijini Dodoma leo tarehe 11 Agosti 2020. Wengine pichani ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndg Beatus Malema (Kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania Dkt Stephan Ngailo (Kushoto).
**************************************
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Katika kuhakikisha kwamba tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo inaongezeka ili kujitosheleza kwa chakula na malighafi za viwandani; Wizara ya Kilimo imeendelea kuhamasisha matumizi ya mbolea ili kufikia kilo 50 za virutubisho kwa hekta moja kama ilivyopendekezwa na wakuu wa nchi za Afrika kupitia Azimio la Abuja la mwaka 2006.
Ili kufikia lengo hilo Wizara yangu ilianzisha Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS – Bulk Procurement System), kufuta tozo mbalimbali za mbolea, kusimamia utaratibu wa usafirishaji wa mbolea na kuweka bei elekezi za mbolea kwa mkulima.
Uingizaji wa mbolea kupitia BPS unahusu mbolea za Urea, DAP, NPK, CAN na SA hivyo BPS imefanya gharama za usafirishaji wa mbolea baharini kushuka kwa kiasi kikubwa kutoka Tshs 23,000/= hadi Tshs 2,350/= Tshs kwa mfuko mmoja wa kilo 50. Hii ni kwa sababu, kabla ya kuanza BPS, kila mfanyabiashara alikuwa akiingiza mbolea bila uratibu na hivyo kufanya meli ziwe zinachukua uzito mdogo kwa wakati mmoja na hivyo gharama za usafiri baharini kuwa kubwa na kusababisha bei za mbolea kwa wakulima kuwa kubwa pia.
Kwa ujumla, bei ya mbolea msimu wa 2020/21 imepungua kwa wastani wa shilingi 1,316 kwa mfuko wa kilo 50 wa UREA ikilinganishwa na msimu wa 2019/20. Kwa upande wa DAP bei imepungua kwa wastani wa shilingi 2,860 kwa mfuko wa kilo 50 ikilinganishwa na msimu wa 2019/20.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga leo tarehe 11 Agosti 2020 ameyasema hayo wakati akitangaza bei mpya ya Mbolea kwa msimu wa mwaka 2020/2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi mdogo wa Wizara ya Kilimo Maarufu kama “Kilimo IV” ofisini kwake Jijini Dodoma.
Amesema kuwa pamoja na punguzo hilo la bei ya mbolea kwa msimu wa 2020/21 ukilinganisha na msimu wa 2019/20, vyama vya ushirika vilivyoshiriki zabuni ya BPS kwa msimu huu wa 2020/21 ambapo vitawauzia mbolea wanachama wao kwa bei nafuu zaidi ya bei elekezi inayotolewa na Serikali, hii ni kutokana na kwamba bei yao haijumuishi faida kama wanavyofanya wafanyabiashara.
Waziri Hasunga amesema kuwa mbolea iliyoagizwa na vyama vya ushirika imewafikia wanachama wao mpaka vijijini walipo.
Kuhusu wastani wa bei ya mbolea ya DAP kitaifa kuanzia leo tarehe 11 Agosti 2020 kwa msimu wa 2020/21 itakuwa shilingi 55,573 kwa mfuko wa kilo 50 ikilinganishwa na shilingi 58,433 kwa mfuko wa kilo 50 msimu wa 2019/20.
Kwa upande wa mbolea ya UREA, wastani wa bei kitaifa kwa msimu wa 2020/21 itakuwa shilingi 48,070 kwa mfuko wa kilo 50 ikilinganishwa na shilingi 49,386 msimu wa 2019/20. Mchanganuo wa bei elekezi za mbolea ya DAP na UREA kwa Mkoa mmoja na mwingine zinatofautiana kutokana na umbali kutoka Dar es Salaam, hali ya barabara na gharama za usafiri.
“Hata hivyo, kwa sasa BPS inatumika kuingiza mbolea za DAP na Urea ambazo zinatumika kwa zaidi ya asilimia 50 ya mbolea zote nchini. Tofauti na miaka mingine ambapo ilizoeleka kwamba waingizaji wa mbolea ni wafanyabiashara peke yake, zabuni za BPS za msimu wa Kilimo 2020/2021 zimeshirikisha vyama vya Ushirika vya wakulima vya Madibila AMCOS na chama kikuu cha wakulima wa mkoa wa Iringa (IFCU – Iringa Farmers Cooperative Union)“ Amesisitiza Waziri Hasunga
Aidha, Mhe Hasunga amebainisha kuwa lengo la kushirikisha vyama vya ushirika ni kupunguza bei za mbolea kwani vyama hivyo vinaingiza mbolea kwa ajili ya matumizi mashambani na sio kutafuta faida kwa kuuza mbolea.
Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS) umeanzishwa kwa lengo la kupata punguzo la bei litokanalo na kununua na kusafirisha mbolea nyingi kwa wakati mmoja (Economies of scale). Tangu kuanza kwa BPS mwaka 2017, huu ni msimu wa nne wa kilimo wa utekelezaji wake ambapo mbolea zimeingizwa nchini kwa punguzo la bei katika chanzo (FOB – Free on Board) kwa asilimia 6 – 17 ikilinganishwa na bei katika soko la Dunia inayosimamiwa na taasisi inayofuatilia bei ya mbolea katika soko la Dunia iitwayo Argus Gmbh.
Zaidi ya asilimia 90 ya mbolea zinazotumika nchini huagizwa kutoka nje ya nchi. Hivyo, katika kutengeneza mjengeko wa bei, gharama mbalimbali huzingatiwa hususani bei ya ununuzi katika chanzo (FOB – Free on Board), bima na usafirishaji wa mbolea baharini, tozo za Mamlaka ya Bandari (TPA) na taasisi mbalimbali za udhibiti, gharama za vifungashio, kufungasha, usafirishaji hadi kwa muuzaji wa rejareja na faida ya mfanyabiashara.
Pia, bei elekezi za mbolea hutegemea umbali wa sehemu inakopelekwa kutokea bandarini. Maeneo yote itakapopelekwa mbolea yana umbali kati ya kilometa 1 na 1,600 kutoka bandari ya Dar es salaam. Kwa Wastani, gharama ya kusafirisha mfuko mmoja wa mbolea wa Kilo 50 kwa barabara kutoka Bandari ya Dar es salaam hadi makao makuu ya Halmashauri kwa barabara ni Sh. 5,500/= kwa kilometa 1,000. Gharama hii hupanda na kushuka kutegemeana na hali ya barabara na hali ya hewa (masika au kiangazi).
“Tofauti na miaka mingine ambapo ilizoeleka kuona wafanyabiashara peke yake wakiingiza mbolea nchini, msimu huu tumeshuhudia wakulima wadogo kupitia vyama vyao vya ushirika wakiwa waingizaji (Importers) wa mbolea kupitia mfumo wa ununuzi wa pamoja (BPS)” Amesema Waziri Hasunga
Ameongeza kuwa katika vyama vyote vya ushirika vilivyotuma maombi, MAMCOS (Madibira Agricultural Marketing Cooperative Society) na IFCU (Iringa Farmers Cooperative Union) ndivyo vilivyoweza kudhaminiwa na Benki ili vipate mbolea kupitia BPS katika zabuni ya kwanza.
Kadhalika, amesema kuwa tayari Wizara ya Kilimo imepokea maombi ya mbolea kutoka vyama vingine na itafanya utaratibu ili navyo vipatiwe mbolea kupitia BPS. Vyama vingine ambavyo havijaleta maombi ya mbolea vitaendelea kupatiwa kwa bei ya punguzo kadri vinavyowasilisha maombi ya mbolea Wizarani kwangu kupitia TFRA.
Waziri Hasunga amesema kuwa pamoja na kuhakikisha kwamba mbolea inayoingia nchini inakwenda moja kwa moja hadi kijijini kusubiri mfumo wa kilimo kuanza, bei ya mbolea imeshuka kwa kiasi kikubwa sana kwa sababu inamfikia mkulima moja kwa moja bila kupitia watu wa kati ambao huweka faida (Tshs 5,000 – 8,000/= kutegemeana na umbali, hali ya barabara na aina ya mbolea) na pia huiuzia maeneo ya mijini yanayofanya mkulima atumie gharama za ziada (Tshs 3,000 – 5,000/=) kuifuata huko na hivyo kuipata kwa gharama kubwa ikilinganishwa na bei elekezi zinazotangazwa.
Hivyo mkulima mdogo aliyeagiza mbolea kupitia BPS ataipata mbolea kwa punguzo la hadi Tshs 10,000/= au zaidi
Bei elekezi kwa mbolea zilizoingizwa na vyama vya ushirika kwa msimu wa 2020/21 zitakuwa shilingi 50,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa DAP na shilingi 43,500 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea aina ya UREA.
MWISHO