Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera Charles akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma leo tarehe 11 Agosti 2020.
……………………………………………………………….
Na.Alex Sonna, Dodoma
Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) imetangaza rasmi kufungwa kwa pazia la uchukuaji wa fomu kwa wagombea wa nafasi ya Urais na Makamu wake katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika siku ya Jumatano Oktoba 28 mwaka huu.
Tamko hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya chaguzi , Dkt. Wilson Mahera Charles wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Jijini Dodoma kwenye Ofisi za Jengo la Uchaguzi House eneo la Njedengwa.
Dk. Charles ameeleza kuwa wamefunga pazia la uchukuaji fomu ulioanza Agosti 5, mwaka huu isipokuwa chama kimoja cha NLD ambacho hakijafanya mkutano hadi Agosti 16, mwaka huu na kinaweza kuchukulia fomu jijini Dar es Salaam
Aidha Dk. Charles amebainisha kuwa vyama vyenye usajili wa kudumu nchini ni 19, na vilivyochukua fomu ni 16 na vyama viwili TLP na UDP havijachukua fomu bali viliahidi kumuuunga mkono mgombea wa urais kupitia tiketi ya CCM Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
“Wote waliochukua fomu si wagombea bali ni watia nia hadi Agosti 25, mwaka huu baada ya Tume kupitia fomu zao ili kujiridhisha kwamba wamekidhi vigezo vya kugombea na ndipo itatoa orodha ya wagombea,”amesisitiza Dk. Charles.
Dk. Charles ameongeza kuwa Agosti 22-25, mwaka huu, Tume itaketi na kupokea fomu za watia nia baada ya kuwa wamepata wadhamini zaidi ya 2000 katika mikoa 10 nchini ikiwamo mikoa nane Bara na miwili visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi kifungu namba 4 (c) Tume ndiyo yenye wajibu wa kutoa elimu kwa mpiga kura kutokana na uchache wa watumishi imealika taasisi za kiraia 245 ili kusaidiana na Tume kutoa elimu hiyo kwa mwongozo wa Tume.