Kaimu Meneja Sehemu ya Uchunguzi(WMA),Bw.Almachius Pastory (kushoto) akihakiki kama pampu ya kujazia mafuta iko vizuri kwaajili ya kutoa huduma kamili kwa wateja. Pembeni yake ni Meneja wa Sheli ya Puma tawi la Ilala Jijini Dar es Salaam Bw.Ibrahim Chalamila akijaza mafuta kwenye chombo maalumu kufahamu kama pampu hiyo ipo vizuri. Stika ya WMA ikitambulisha Pampu kama imekaguliwa na Wakala wa Vipimo na kuwa tayari kwaajili ya kutoa huduma kwa wateja. Kaimu Meneja Sehemu ya Uchunguzi(WMA),Bw.Almachius Pastory akishuhudia wahudumu wa sheli ya PUMA wakiwahudumia wateja walioweza kufika. Kaimu Meneja Sehemu ya Uchunguzi(WMA),Bw.Almachius Pastory akionesha stika ya WMA ambayo inatambulisha kwamba pampu hiyo ya mafuta imekaguliwa na inafaa kwa kutoa huduma.
************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Wananchi wametakiwa kuhakiki pampu za kujazia mafuta (Sheli)kama zina stika ya Wakala wa Vipimo (WMA) ili kuweza kuwekewa mafuta kwa kiwango unachohitaji.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam,Kaimu Meneja Sehemu ya Uchunguzi (WMA), Bw.Almachius Pastory ili kuweza kutambua pampu za kujazia mafuta zimekaguliwa na WMA lazima ziwe na stika ya WMA ambayo inaonesha tarehe ya ukaguzi mpaka lini inatakiwa ikaguliwe tena.
“Pampu zote ambazo zimekaguliwa zinakuwa na stika ambazo zimeelezea mwaka zimekaguliwa lini na zinatarajia kukaguliwa lini kwahiyo kituo chochote ambacho pampu zake hazina stika basi sio sahihi hazijakaguliwa ama zimebanduliwa kwasababu hazitakiwi kutumika.Mteja anatakiwa kabla hajahudumiwa aangalia stika ya WMA pale mbele kwenye pampu ya kujazia mafuta”.Amesema Bw.Pastory.
Aidha Bw.Pastory amesema ukaguzi wa kawaida huwa huwa wanafanya baada ya mwaka mmoja, pia wanafanya ukaguzi wa kushtukiza mara kwa mara na atakae kutwa na tatizo atapigwa faini au kupelekwa mahakamani.
“Kituo chochote cha mafuta ambacho hakina nembo ama stika ya WMA akitakiwi kufanya kazi kwahiyo atakuwa kinyume na sheria ya Wakala wa Vipimo”. Ameongeza Bw.Pastory.
Pamoja na hayo Bw.Pastory amesema kuwa wao wanajukumu la kuhakikisha kwamba kinachotoka ndicho anachopata mteja ili isitokee wizi wa mafuta bila mteja kufahamu.
Nae Meneja wa Sheli ya Puma tawi la Ilala Jijini Dar es Salaam Bw.Ibrahim Chalamila amesema WMA kufanya uhakiki kwa pampu za mafuta ni jambo zuri kwani inasaidia kuwatoa wasiwasi wateja wao ambao wanafika kwaajili ya kuhudumiwa mafuta.
“Kuna baadhi ya wateja hapo nyuma huwa wanakuja hapa huku wakiwa na wasiwasi na mashine zetu hivyo kwa kipindi hiki ambacho WMA wanapitia pampu zetu na kuwapatia wateja wetu elimu wanatuweka sisi salama kwa wateja wetu”. Amesema Bw.Chalamila.
Hata hivyo amewataka wateja wawe makini pale wanapoapatiwa lisiti halali kwani wanatakiwa kuhakikisha lisiti inatoka kwenye mashine.
Kwa upande wa Wateja wa Mafuta wamesema kuwa elimu hiyo hawana hivyo kwasasa wataendelea kuwaelimisha na wengine kufahamu umuhimu wa kuangalia pampu za mafuta kabla ya hawajahudumiwa ili kuweza kuwekewa mafuta kwa kiasi ambacho wanahitaji.
“Wahusika wangekuwa wameshatuelimisha mapema kuhusu umuhimu wa kufahamu pampu ambazo zimeshakaguliwa na kukidhi viwango ambavyo ni halali kwaajili ya kumuhudumia mteja pasipo kuibiwa mafuta basi wengi tusingekuwa tunaibiwa ila kwasasa nashukuru nimepata uelewa huu” Amesema Mohamed Kija dereva wa bodaboda.