************************************
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
Agost 11
SERIKALI Wilaya ya Bagamoyo ,Mkoa wa Pwani, imefanikiwa kutatua kero za mnada, nyumba ya mganga na mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Ruvu Darajani na Ranchi ya Ruvu iliyoko jirani na kijiji hicho.
Hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli, inayolenga kutatua kero zinazowakabili wananchi wake hususani wa hali ya chini, ambao wamekuwa kwenye malalamiko tofauti yanayohusiana na sekta mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainab Kawawa, akiwa ziarani kwenye Vijiji vya Ruvu Darajani, Mbala Kijiweni na Milo Kata ya Vigwaza ,Chalinze, alisema serikali inajivunia kutatua changamoto hizo ambazo zilikuwa kero kwa jamii.
Alisema,baada ya kuteuliwa nafasi hiyo alifika kijijini hapo ambapo alikuta kero za kufungwa mnada, kutomalizika nyumba ya Mganga ikiwemo mpaka ambapo zote zimeshapata ufumbuzi.
“Unaweza ukakufuru mungu hakupi unachokiomba kumbe hujashukuru, kwanza tushukuru kwa kazi ambayo imeshafanyika ndipo tuendelee na hayo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ambayo yapo kwasasa,” alisema Kawawa.
Akiwa Ruvu amepokea kero za wakazi kutoka nje ya Ruvu kujipenyeza kutaka ardhi iliyotolewa na Rais Dkt. John Magufuli, kupitia Wizara ya Mifugo chini ya Ranchi ya Ruvu kwa ajili ya wakazi hao, huku wakazi wa Milo wakilalamikia mifugo kupita kwenye mashamba yao inapokwenda kunywa maji.
Awali Mwenyekiti wa Kijiji ,Rashid Gama alimwambia Kawawa kuwa wakazi waliojitambulisha wanalima ndani ya Kijiji hicho hawatambui na ofisi haiwatambui.
Kutokana na kauli ya Gama iliyothibitisha kuwepo kwa uvamizi huo, Kawawa alimuagiza Mkuu wa Polisi Chalinze (OCD) SP Hussein Mdoe, akawahoji mkazi aliyesema wanatokea Mlandizi wanalima Ruvu wakati Kijiji hakiwatambui huku Mathayo Kisweswe Mwenyekiti wa Kitongoji cha Relini akidaiwa kupokea pesa pasipo risiti.