Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Shinyanga
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga Leo tarehe 10 Agosti 2020 amefanya ziara ya kikazi mkoani Shinyanga ambapo amekagua na kuridhishwa na hali ya ununuzi wa msimu wa Pamba kwa mwaka 2020/2021.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda cha kuchambua Pamba cha Afrisian, Aham, GAKI na Fresho Waziri Hasunga amewapongeza wamiliki wa kampuni hizo kwa mapokezi mazuri ya Pamba pamoja na kuwalipa wakulima kwa wakati.
Akizungumzia mfumo wa malipo ya Taslimu na Benki Amesema kuwa mifumo hiyo inaendelea kufanyiwa kazi ili kuona mfumo upi utakuwa na ubora zaidi kwa wakulima na wanunuzi.
Amesema kuwa serikali haitopanga bei elekezi ya mazao ya wakulima badala yake itaacha soko liamue. “Hatuwezi kumpangia bei mkulima kwani hatukumsaidia kuandaa shamba, kulima na hata kupalilia. Kwanini sasa hivi ameshavuna ndio tumuingilie hilo sio sahihi” Alisisitiza
Pia, Waziri Hasunga ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kusimamia kwa weledi mkubwa sekta ya kilimo jambo lililopelekea kuwa na ziada ya kutosha ya chakula.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe Jasinta Mboneko amempongeza Waziri wa Kilimo kwa kufanya ziara ya kikazi katika mkoa huo huku akibainisha kuwa wakulima wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na kukumbwa na changamoto ya mvua kuzidi lakini wamelima Pamba yenye ubora wa kutosha.
Kadhalika, ametoa mwito kwa wakulima kuendelea kuzitoa Pamba zao majumbani na kuzipeleka kwenye viwanda vya kuchakata Pamba ili kujipatia kipato chao ili waweze kuboresha mazingira ya maisha yao.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Ndg Albert Msovela amesema kuwa msimu wa Pamba mkoani hapo ulizinduliwa tarehe 15 Juni 2020 wilayani Nzega ambapo tangu wakati huo wanunuzi wamekuwa wakifurahishwa na ubora wa Pamba huku wakulima wakipatiwa malipo yao kwa wakati.
MWISHO