Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Busega ambaye pia ni msimamizi wa uchaguzi jimbo la Busega, Anderson Njiginya Kabuko (kushoto) akisoma taratibu na maadili ya uchaguzi, wakati semina ya mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata.
…………………………….
Kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata jimbo la Busega wamekula viapo vya kutunza siri na kujitoa uanachama wa vyama vya siasa, huku msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, Ndg. Anderson Njiginya Kabuko amewataka wasimamizi wasaidizi hao ngazi ya kata kuzingatia viapo walivyoapa.
Ndg. Kabuko ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Busega amefungua semina ya mafunzo hayo ya siku tatu ambayo yalianza tarehe 7 hadi 9/8/2020 amewataka wasimamizi wasaidizi kupokea mafunzo hayo kuwa makini na kujifunza kwa vitendo hatua mbalimbali.
Aidha amewataka wasiwe chanzo cha changamoto au matatizo kwenye zoezi hili la uchaguzi mwaka huu. Pia amewataka kuzingatia maadili yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili zoezi hili la uchaguzi wa mwaka huu uende salama na kuwataka wasiwe na ushabiki wa vyama.
Wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata wametakiwa kuwa na utiifu na utunzaji wa siri ili kufanikisha lengo. Katika mafunzo hayo yaliyohudhuliwa pia na Afisa Uchaguzi wa Wilaya ya Busega Bi. Grace Ishongoma amewaomba wasimamizi wasaidizi hao kuwa makini wakati wote wa zoezi la uchaguzi kwa kila hatua itakayokuwa inaendelea.
Wasimamizi wasaidizi hao waliapishwa na Hakim Mkazi, Mahakama ya Mwanzo Ndg. Alex Ombusso na kuweza kujaza fomu namba 6 na 7, ambazo zinawataka kutunzwa kwa siri na kujitoa uanachama wa vyama vya siasa. Uchaguzi mkuu wa mwaka huu unatarajia kufanyika tarehe 28/10/2020 kwa ngazi ya Rais, Wabunge na Madiwani.
Wasimamizi wasaidizi hao wa ngazi ya kata ambao wameshiriki semina hiyo wamefurahishwa na mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi mambo yote waliyojifunza ili uchaguzi uwe wa amani katika kipindi chote cha uchaguzi.