Jioni ya leo Senzo ameandika taarifa ya kujiuzulu Simba SC kupitia akaunti yake ya Twitter baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa muda mfupi na kwa mafanikio.
Senzo ameushukuru uongozi wa Simba SC kwa kumpa fursa ya kuiongoza klabu hiyo kubwa na anajivunia mafanikio aliyowaachia ndani ya muda mfupi ikiwemo kushinda mataji yote matatu msimu huu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu ya Tanzana Bara na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).
Baada ya taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, Mohamed ‘Mo’ Dewji naye akaandika;
“Tumetoka mbali na bado safari inaendelea, tumepita mengi Wanasimba wenzangu. Nawaomba Wanasimba wote mtulie. Simba SC ni kubwa kuliko mtu mmoja. Sisi viongozi tunawatumikia usiku na mchana bila kujali maslahi ya mtu binafsi bali Simba. Kazi inaendelea, tuko imara,”.
ikafuatia taarifa rasmi ya klabu ikisema kwamba imesikitishwa na taarifa za ghafla za kujuzulu kwa Senzo na kumtaka aende kukabidhi ofisi haraka iwezekanavyo.
“Bodi ya klabu ya Simba imemtaka ajieleze kuhusu mambo ambayo hayajakamilika na kufanya makabidhiano kwa weledi haraka iwezekanavyo,”.
Aidha, taarifa hiyo imewataka wanachama na wapenzi wa Simba SC kuendelea kuwa watulivu hadi hapo atakapotangazwa Kaimu Mtendaji Mkuu.
Tayari kuna picha inasambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Senzo akiwa na vigogo wa klabu ya Yanga, Mhandisi Hersi Said, Karigo Godson na Philemon Ntahilaja akisaini fomu.
Senzo aliajiriwa Simba SC Septemba 7, mwaka jana akichukua nafasi ya Crescentius John Magori aliyejiuzulu pia na ndani ya muda mfupi amefanya klabu iweze kujiendesha kwa weledi na kufanikisha mambo mengi ndani na nje ya Uwanja.
Kabla ya kuja Simba, Mazingisa amezitumikia klabu za Platinum Stars, Orlando Pirates katika nafasi mbalimbali za utendaji pamoja na na Shirikisho la Soka Afrika Kusini (SAFA).
Senzo Mazingisa (kushoto) aliajiriwa Simba SC Septemba mwaka jana akichukua nafasi ya Crescentius Magori (kulia)