Home Mchanganyiko JIJI LA DODOMA MSHINDI MAONESHO YA 88 KANDA YA KATI

JIJI LA DODOMA MSHINDI MAONESHO YA 88 KANDA YA KATI

0

Mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (watu wenye ulemavu), Stella Ikupa akimkabidhi cheti cha ushindi wa kwanza kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma, Katibu Tawama Wilaya ya Dodoma Mjini, Michel Maganga akipokea cheti ya ushiri wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika maonesho ya 27 ya Nanenane jijini Dodoma. 

Wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika picha ya pamoja muda mfupi baada ya kupokea cheti ya ushindi wa kwanza kwa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kwenye maonesho ya 27 ya Nanenane yaliyofanyika katika uwanja wa Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma

…………………………………………………………………………………

Na.Mwaandishi Wetu,Dodoma

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeendelea kushika nafasi ya kwanza katika maonesho ya Nanenane kanda ya kati kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kutokana na ushirikiano wa kitaasisi na wadau wengine katika kufikisha teknolojia kwa wananchi. 

Akiongea wakati wa kutoa zawadi kwa washindi, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Stella Ikupa aliyemuwakilisha ngeni rasmi Waziri wa Sheria na Katiba, Mwiguli Nchemba aliwapongeza washindi. 

Mgeni rasmi Ikupa alisema “niwashukuru na kuwapongeza sana washindi wote kutokana na kazi nzuri mliyoifanya hadi kupata ushindi huu”. Aidha, aliwataka kuendelea kuwa mfano mzuri katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwawezesha wananchi kukua kiuchumi.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeibuka mshindi ikizishinda Halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma katika eneo la maonesho ya mabanda kwa Halmashauri. 

Akiongelea ushindi huo, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA na Uhusiano katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alisema kuwa ushindi huo ni kielelezo cha dhamira thabiti ya Halmashauri kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wa Jiji hilo ili kuwasaidia kukuza uchumi. “Halmashauri ya Jiji baada ya kupewa hadhi ya kuwa Jiji na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli, vijiji vyote vimefutwa na hivi sasa Jiji lina mitaa 222. Hivyo, basi tumejipanga kuhakikisha katika Jiji la Dodoma tunafanya kilimo cha mjini. Katika Mpango Kabambe (Master Plan) wa Jiji, yametengwa maeneo maalum kwa ajili ya kilimo cha mjini. Kwa muktadha huo, Jiji limekuwa na mkakati wa kuhakikisha linatoa elimu ya kilimo, na ufugaji wa kisasa kwa kutumia teknolojia za kisasa. Hiki ndicho tumefanya katika maonesho ya 27 ya Nanenane mwaka huu na ushindi wetu ni uthibitisho kuwa mikakati ya lengo letu imeanza vizuri” alisema Fungo.

Akiongelea maonesho hayo, alisema kuwa Halmashauri hiyo ilionesha teknolojia za umwagiliaji kwa kutumia miundombinu ya umwagiliaji wa matone, usindikaji na uhifadhi wa bidhaa kwa kutumia vifungashio vyenye ubora na mbinu za ufugaji wa kisasa na uandaaji wa malisho ya mifugo. Maeneo mengine aliyataja kuwa ni ufugaji samaki wa kisasa na nyuki. 

Vilevile, kulikuwa na maonesho ya kilimo cha mbogamboga, matunda na mazao ya nafaka kwa kutumia mbinu za kisasa, aliongeza.

Fungo alitoa wito kwa wananchi wa Jiji hilo kuendelea kutumia fursa hiyo adhimu ya kupata mbinu za kilimo na ufugaji wa kisasa katika mazingira ya Jiji. “Jiji linao wataalam wa kutosha na katika banda letu hapa Nanenane tutaendelea kuonesha na kufundisha mbinu hizo kwa muda wote kama ilivyoagizwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Mheshimiwa Selemani Jafo.

Katika maonesho ya 27 ya Nanenane Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilishika nafasi ya kwanza ikiwa ni mwaka wa pili mfululizo, Halmshauri ya Wilaya ya Kondoa ilishika nafasi ya pili na Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa nafasi ya tatu, washindi wote walizawadiwa vyeti.